ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, November 29, 2022

KATIBU MKUU TIXON NZUNDA AFUNGUA JENGO LA TVLA IRINGA.

 

Katibu mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Tixon Nzunda akiongea wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kilichopo eneo la Isoka Machinjioni mkoani Iringa kinachotarajiwa kuhudumia wafugaji wote waliopo kanda ya nyanda za juu kusini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (katikati) akifanya tukio la ufunguzi wa jengo jipya la la Maabara na Ofisi, Kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kinachohudumia wafugaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,Kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi na kushoto kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada.Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi akiongea wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kilichopo eneo la Isoka Machinjioni mkoani Iringa kinachotarajiwa kuhudumia wafugaji wote waliopo kanda ya nyanda za juu kusini.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

KATIBU mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Tixon Nzunda amefungua jengo jipya la kituo cha Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kilichopo eneo la Isoka Machinjioni mkoani Iringa kinachotarajiwa kuhudumia wafugaji wote waliopo kanda ya nyanda za juu kusini.

 

Akizungumzia wakati wa kuzidua jengo jipya la Wakala hiyo, Nzunda aliwataka viongozi wa Mkoa wa Iringa kuwahamasisha wananchi na wafugaji wote kutumia huduma zinazotolewa kituoni hapo ili waweze kuboresha mifugo yao na kukuza uchumi wa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Nzunda alisema kuwa sasa ni wakati wa kufuga kisayansi na ndio maana TVLA walewaletea kituo hicho ili kuwasaidia kutekeleza shughuli za ufugaji wa kisasa kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia yaliyopo ulimwenguni kote hasa kupitia mfumo mpya wa kidijitali wa kusajili viuatilifu vya mifugo, ufuatiliaji, uzalishaji na usambazaji wa chanjo unaotumiwa na TVLA kwa sasa na kwa hili niwapongeze sana kwani mtapunguza upotevu wa mapato na kurahisisha sana utendaji wenu.

 

Alisema kuwa anawapongeza wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kwa ubunifu wa kuadhimisha wiki maalum ya wakala hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya kuanzishwa kwake na kufana kwa kwa kuwa na ubunifu mkubwa katika kuwahudumia wananchi.

 

 

 Nzunda alimuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga kuweka utaratibu wa kuanzisha wiki ya Mifugo kuanzia mwaka ujao wa fedha ambayo itazishirikisha Taasisi zote za Serikali zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo pamoja na zile zilizopo Sekretariati za Mikoa, mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau kutoka Sekta binafsi.



“Ubunifu huu ndio mtazamo wa Wizara kwa sasa na kwa kufanya hivi sio tu tumeweza kutangaza shughuli za taasisi bali tumefanikiwa kuelimisha UMMA na kufanya mawasiliano ya karibu na jamii tunayoihudumia kupitia vyombo vya habari, vikundi mbalimbali na mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Tovuti ya Wakala na ninaamini Taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara zitaiga jambo hili” Ameongeza Nzunda.



Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Stella Bitanyi alisema kuwa katika kipindi cha Wiki moja ya Maadhimisho hayo, Wakala hiyo imefanikiwa kutoa bure dozi 150,000 za chanjo ya magonjwa ya Kimeta, Mdondo, Homa ya mapafu ya Mbuzi/Ng’ombe, Chambavu na Kutupa mimba zenye thamani ya zaidi ya Tshs.Mil.5 Kutembelea viwanda 50 vinavyozalisha vyakula vya Mifugo ili kutoa elimu ya uhakiki wa ubora wa vyakula vinavyozalishwa, kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa.

 

Dkt. Bitanyi alisema kuwa wakala hiyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kutembelea na kutoa misaada kwa wasiojiweza na kwenye vituo 7 vya Watoto yatima vilivyopo maeneo mbalimbali hapa nchini, kufanya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo bure kwenye sampuli 400 za wanyama mbalimbali katika maabara za Wakala, kutoa huduma za uogeshaji bure kwa Mbwa 200 na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma ya usajili na uchambuzi wa ubora wa viuatilifu vya Mifugo ambayo sasa inatolewa na Wakala hiyo kupitia vituo vyake vyote nchini.



Alisema kuwa wakala katika kutekeleza majukumu kwa kipindi cha miaka 10 wanajivunia mafanikio waliyopata katika kutoa huduma na bidhaa za kiveterinari na Kuongezeka vituo 2 vya maabara kutoka vituo 11 mwaka 2012 hadi 13 mwaka 2022, Kupatikana kwa Ithibati (accreditation) katika uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo kulingana na kanuni za kimataifa, kuongeza mapato ya ndani kutoka milioni 220 hadi bilioni 3.1 kwa mwaka 2022, na kujengea uwezo maabara ya kupima ubora wa vyakula vya mifugo, kuangamiza Mbung’o wanaoeneza ugonjwa wa Nagana kwa Ng’ombe na Malale kwa binadamu pamoja na Kupewa jukumu jipya la kusajili na kuthibitisha ubora wa viuatilifu vya mifugo kuanzia mwezi Julai 2022” Ameongeza Dkt. Bitanyi.



Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Elias Luvanda alisema kuwa anaishukuru Wizara kwa kuamua kujenga Kituo cha Wakala hiyo mkoani Iringa.

 

luvanda alisema kuwa kituo hicho kimejengwa mahali sahihi kwani mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya Mifugo ambapo mpaka sasa una takribani mifugo Mil. 8.7 ambayo inajumuisha Ngombe Mbuzi, Kondoo, Nguruwe, Punda, Kuku, Mbwa na Paka.



Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa ambako ndipo kilipojengwa kituo hicho Ibrahim Ngwada alisema kuwa Halmashauri itaendelea kuweka mazingira Wezeshi kwa Serikali kutekeleza miradi yake ambapo ameahidi kufikisha kwenye vikao vyao vya kisheria suala la lililokuwa eneo la Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini lililochukuliwa na Halmashauri hiyo ili lirejeshwe kwa wakala hiyo jambo ambalo litaiwezesha kupanua wigo wa huduma zake.

 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.