ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, October 21, 2022

RAO PWANI AKEMEA VITENDO VYA WAZAZI KUWABAGUA WALEMAVU KATIKA KUPATA ELIMU

 

Afisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki akizungumza wakati wa kufunga rasmi mafunzo hayo ya siku Tano kwa walimu wa MJM .


 Baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja wakionyesha kile walichofundishwa kwa muda wa siku tano.

Na Victor Masangu,Bagamoyo.

Afisa elimu Mkoa wa Pwani  Sara Mlaki amewataka wazazi na walezi kuachana na tabia ya kuwaficha na kuwafungia ndani watoto wao wenye ulemavu na badala yake watumie vituo vya utayari 36 ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya kwenda kuwaandikisha kupata elimu ya awali ili kuwaandaa na kujiunga na darasa la kwanza mwaka 2023.


Aidha afisa elimu huyo amewaasa walimu Jamiii Wasaidizi (MJM) ambao wemepatiwa mafunzo kwenda kuwaangalia kwa namna ya kipekee  watoto wenye ulemavu wasibaguliwe na kupatiwa haki yao ya msingi katika kupata elimu kama wengine.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa kufunga Mafunzo ya siku Tano Kwa Walimu Jamiii Wasaidizi(MJM) wapatao 38 kutoka halmashauri zote tisa zilizopo katika Mkoa wa Pwani yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufundisha watoto  wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 9.

Alisema kwamba watoto wote ambao ni walemavu na wamefikia umri wa kuanza shule ya awali  katika Mkoa wa Pwani wanapaswa kupatiwa haki zao zote za msingi kama ilivyokuwa kwa watoto wengine kupatiwa elimu  bila ya kuwa na ubaguzi wowote.

Pia alisema kwamba walimu hao waliohitumu mafunzo kwa kushirikiana na jamii husika wanatakiwa kuhakikisha wanaweka mipango mizuri katika vituo hivyo vya utayari ili kusiwe na upendeleo wowote na kila mtoto aweze kupata elimu hiyo ya awali.

"Walimu wa MJM ambao mmepatiwa mafunzo haya ni lazima mkayafanyie kazi kwa vitendo katika vituo vya utayari ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya kuwasaidia watoto kupata elimu ya awali,"

 "Ninawaomba wazazi na walezi kuachana kabisa na vitendo vya kuwaficha na kuwafungia ndani  watoto ambao ni walemavu na badala yake wawape fursa ya kuwapeleka kupata elimu ,"alifafanua Mlaki

Kadhalika aliwakumbusha walimu hao waliohitumu mafunzo ya MJM kutekeleza majukumu yao ipasavyo kama walivyofundishwa na kwamba watoe ushirikiano wa kutosha kwa wazazi pamoja na jamii katika suala zima la kuwaandikisha watoto wao katika vituo hivyo vya utayari.

Naye mmoja wa  wawezeshaji katika  mafunzo akiwamo Hellen Kulwa alisema kuwa  kupitia Mafunzo waliyoyatoa Kwa MJM  hao Katika kuzingatia mahitaji maalumu ya wanafunzi Wenye Ulemavu Wana hakika watayafanyia kazi ipasavyo hasa Katika kutumia mbinu walizofundishwa.

Nao baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo walisema kwamba watakwenda kuyatumia vizuri mafunzo ambayo wameyapata na kuahidi kuyafanyia kazi bila ubaguzi wowote yale yote ambayo yameelekezwa kwa kipindi cha muda wa siku tano.

 Mafunzo hayo ya siku Tano walimu wa MJM wameweza kufundishwa kutengeneza dhana  za Darasani  Ikiwamo mipira ,Vikombe Kwa kutumia karatasi Kuandika herufi kwa kutumia Mbegu na kuandaa Kona za Hesabu,Michezo ,Mazingira na Kona za Nyumbani.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.