Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sarah Msafiri akimkabidhi nahodha wa timu ya New generation kombe baada ya kuutwa ubingwa huo.
Na Victor Masangu,Kibaha
Timu ya soka ya New generation Leo imeweza kuibuka kidedea kwa kuutwa ubingwa wa michuano ya kombe la 'Samia Suluhu Cup' baada ya kuichapa timu ya Palasupalasu kwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa katika dimba la mwendapole Wilayani Kibaha.
Katika mchezo huo wa fainali ambao ulikuwa wa vuta ni kuvute kutokana na timu zote mbili kuonyesha kandanda la aina yake katika kipindi chote cha dakika 90 na kuhudhuliwa na umati wa mashabiki kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Kibaha na maeneo mengine ya jirani.
Mchezo huo ambao ulikuwa unasubiliwa kwa hamu na shauku kubwa na wapenzi wa mpira wa kandanda ulihudhuliwa pia na viongozi mbali mbali wa dini,serikali,pamoja na wadau wa viongozi wa chama Cha mpira wa miguu wilaya ya Kibaha (KIBAFA)
Mabingwa katika mchezo huo ndio waliokuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za wapinzani wao katika kipindi Cha kwanza ambapo bao lao la kwanza lilifungwa kwa njia ya kawaida na bao la pili lilifungwa kwa njia ya mkwaju wa penati.
Katika kipindi c ha pili wapinzani wao waliweza kupata bao la kufutia machozi ambalo lilipatikana kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wao kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sarah Msafiri ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele Cha michuano hiyo ambapo alisema lengo kubwa ya kuandaa mashindano hayo kupitia sekta ya michezo ni kwa ajili ya kuhamasisha zoezi la sensa ya watu na makazi.
"Tunashukuru mashindano haya ya Samia Suluhu Cup' katika Wilaya yangu ya Kibaha yamemalizika salama na kikubwa ilikuwa ni kuwakutanisha wanamichezo kuwahamasisha kushiriki katika sensa na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa ,"alisema Msafiri.
Aidha Mkuu huyo alisema kwamba katika michuano hiyo imeweza kusaidia kwa kiasi kubwa tangu ilipoanza kufanyika na imeleta matokeo chanya katika kuwaimisha wananchi na wanamichezo umuhimu wa kuhesabiwa katika sensa.
Msafiri aliwapongeza wachezaji wa timu mbali mbali ambao wameweza kujitokeza katika mashindano hayo ya Samia Suluhu Cup' na kwamba yatakuwa yanafanyika kila mwaka lengo ikiwa pia ni kukuza vipajj.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji Kibaha Injinia Mshamu Munde amebainisha kwamba Maandalizi yote kwa ajili ya sensa yanaendelea vizuri na kwamba hamasa na mwamko kwa wananchi no mkubwa.
Munde aliongeza kuwa mashindano ya michezo ambayo yameandaliwa maalumu kwa ajili ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi yameleta matokeo chanya katika suala zima la kuwapa fursa wanamichezo kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.
Kivumbi Cha michuano hiyo Cha kombe la Samia Suluhu Hassan kimemalizika ambapo timu za soka kuanzia mshindi wa kwanza hadi mshindi wa nne zimeoatiwa zawadi mbali mbali ikiwemo mipira,jezi, medani pamoj vikombe.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.