Bertha Ismail.
Arusha . Zaidi ya wananchi 40,000 kutoka vijijini saba vya Tarafa ya Meserani wanatarajia kuanza kunywa maji safi na salama baada ya serikali jana kumkabidhi mkandarasi mradi wa kuanza ujenzi wa miundo mbinu ya maji itakayogharimu jumla ya bilioni 1.7.
Hatua hiyo imefikia baada ya hivi karibuni wananchi hao kuandamana hadi barabarani na kuzuia msafara wa waziri wa Maji Jumaa Aweso aliyekuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji agost 1 mwaka huu.
Wananchi hao walimlilia wakiwa na ndoo kichwani wakidai kuwa wamechoka kutembea umbali mrefu kusaka maji ya mabwawa na vidimbwi kwa matumizi ya nyumbani ikiwemo kunywa hali inayopelekea kuugua kila kukicha.
Akizungumza katika kamabidhiano hayo, meneja wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini ‘RUWASA’ Neville Msaki alisema kuwa maandamano yenu yamezaa matunda ya kufanikisha serikali kupitisha bajeti ya bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji katika vijiji saba vya kata ya Esilalei na majengo.
“Baada tu ya kupokea fedha hizi, serikalii ilituagiza kumtafuta mkandarasi haraka na kusaini mkataba ambavyo vyote tiyari na kama mnavyoomuona tumekuja kwenu kumtambulisha na kumkabidhi eneo la mradi ambapo anaanza kazi kesho ya kusambaza mabomba na kuhakikisha anaukamilisha mradi na kuukabidhi baada ya miezi sita ukiwa na mafanikio ya wananchi kuanza kutumia maji safi” alisema Msaki.
Alisema kuwa mradi huo unaotoa maji kutoka chanzo cha mto wa Mbu unatarajia kutoa kiasi cha lita milioni moja kwa siku ambayo yanatosha kwa matumizi ya kawaida ya wananchi wote wa vijiji hivyo na vya jirani.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi mkandarasi eneo hilo la kuanza mradi, mkuu wa wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe alisema kuwa mradi huo uliokuwa uanze siku nyingi ulikwama kutokana na fedha hazikufika hivyo ziara ya waziri imeleta mafanikio hayo.
“leo mradi unaanza ni mafanikio makubwa sana hivyo nimualike afisa wa TAKUKURU hapa na kamanda wa polisi wilaya washirikiane na wataalamu hawa mradi ukamilike ndani ya muda, kwani wananchi hawahitaji siasa bali maji pekee na sitaki kuja kusikia kuna mahali nyumba zimerukwa hazina maji, hakika hatutaelewana” alisema Mwaisumbe
Mwaisumbe pia alimtaka meneja wa RUWASA kuzivunja jumuiya zote za watumia maji zilizopo na kuunda chombo kimoja ndani ya siku 21 kitakachosimamia miradi yote ya maji ili kurahisisha ufuatiliaji na uwajibika katika utendaji na utekelezaji.
Nae mwenyekiti wa baraza la halmashauri ya Monduli, Isack Kadogoo alishukuru serikali kwa mradi huo na kuwataka wananchi hao kutoa ushirikiano wa ulinzi wa vifaa na miundombinu ya mradi visiibiwe.
“Tumemuomba mkandarasi vibarua wote watoke hapa eneo la mradi ili hata mama zetu wapike chakula wauze lakini na nyie mtoe ushirikiano mzuri wa kutunza na kulinda hivi vifaa, jamani msiibe tukaanza kukamatana na vyombo vya sheria tukachelewa kunywa maji mazuri”
Nae mkandarasi huyo, Fauz Eshaq kutoka kampuni ya ‘Skywords construction Ltd’ alisema kuwa amepokea mradi na kuahidi kuutekeleza ndani ya mda kwa uaminifu mkubwa hivyo kuomba ushirikiano wa karibu na viongozi wa serikali wa ngazi zote za vijiji hadi wilaya.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.