ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 22, 2022

WASIOENDELEZA MASHAMBA YA MKONGE KUNYANG'ANYWA

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona


*****************

Muheza, Tanga
Serikali imesema watu waliopewa mashamba katika Shamba la Mkonge la Kibaranga (Kibaranga Sisal Estate) lililoko Muheza mkoani Tanga na hawajayaendeleza au wameyaendeleza kwa mazao mengine watanyang’anywa.

Shamba hilo lenye Hekta 5,600 ambalo linamilikiwa na Bodi ya Mkonge na kusimamiwa na Amcos ya Kibaranga baada ya serikali kulirudisha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ambao walionyesha kusua sua katika uendelezaji wa shamba hilo. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema hayo jana katika kikao na viongozi wa Chama cha Ushirika wa Mazao na Masoko (Amcos) cha Kibaranga na wa kijiji ambapo pamoja na mambo mengine wananchi walitaka kujua utaratibu wa kuendeleza maeneo hayo kwa ujenzi wa nyumba.

Hoja hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kibaranga Amcos, Paulo Haule ambaye alisema amepata maombi ya wananchi wananchi katika eneo hilo wakitaka kujenga makazi ndani na pembezoni mwa shamba hilo.

Akijibu hoja hiyo, Kambona alisema shamba hilo liligawiwa eka tatu kwa kila mkulima ili walime na kuendeleza zao la mkonge lakini wengine wamefanya kilimo cha mazao mengine kinyume na makubaliano.

“Labda niwakumbushe tu hili shamba linaitwa Kibaranga Sisal Estate, ni shamba la mkonge si shamba la michungwa. Lakini pia niwaambie wakazi wa Muheza popote walipo wajue kuwa hawajapewa hizi ardhi ili wajenge nyumba, walipewa zile eka tatu tatu ekari moja ulime mkonge halafu ndiyo upande mazao yako mengine.

“Tunafahamu Mheshimiwa Waziri Mkuu amefika hapa mara tatu na mara zote amesisitiza suala la uongezaji wa uzalishaji na ndiyo sababu ya shamba hili kurudishwa Bodi ya Mkonge baada ya kuonekana kuwa tangu imekaa halmashauri hakuna uendelezaji wa kilimo cha mkonge uliofanyika kuanzia shamba lenyewe na mashine ambayo inatakiwa ifufuliwe ili ianze kuchakata mkonge.  

“Kwa hiyo serikali imesema shamba lirudi Bodi ya Mkonge na bodi iratibu shughuli za uendelezaji wa hili shamba,” alisema Kambona.

Alisema Bodi ya Mkonge ikishirikiana na Amcos ya Kibaranga ambayo ni moja ya Amcos changa lakini zinakuja vizuri kwa sababu ya umadhubuti wa uongozi ambapo wanashirikiana nao vizuri wakisaidia ugawaji kwa maana ya kuleta hali ya utulivu kwenye shamba hilo na kuhakikisha wanaratibu masoko ya mkonge kwa wale waliofikia hatua ya kuvuna.

“Sasa niwaambie tu wananchi wa Kibaranga, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo wakati amekuja tu mwaka jana alifanya kikao hapa na akarejea maagizo ya Waziri Mkuu kwamba waliopewa mashamba hapa walime mkonge, hili ni shamba la mkonge kwa hiyo walime mkonge.

“Kama umepewa shamba na hujaliendeleza, shamba hilo utanyang’anywa na kupewa mtu mwingine ambaye yuko tayari kulima mkonge. Kwa hiyo isikupe sifa kwamba mimi ninayo hati halafu una miaka sita tangu upewe hilo shamba hujaendeleza kwa kilimo cha mkonge,” alisema.

Aidha, Kambona alisema Bodi itatoa tarehe ambayo ikivuka hiyo tarehe mashamba hayo yote yataanza kugawiwa upya kwani hawataki kuona mapori wanataka kuona mkonge ukiwa umeshamiri.

Alisema shamba hilo ni kubwa ambapo likipandwa mkonge tayari linakuwa limeshafikia lengo la serikali kwa asilimia kubwa kwani litakuwa limeongeza uzalishaji kuelekea tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

“Kwa hiyo wananchi watambue hivyo na serikali iko makini sana ni kweli wale ambao hawataendeleza mashamba yao kwa kilimo cha mkonge tutawanyang’anya, umepanda machungwa ndani ya shamba la Kibaranga tutakunyang’anya hilo eneo tumpe mtu mwingine,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Kambona alisema Wilaya ya Muheza ina ardhi nzuri kwa kilimo cha machungwa nje ya shamba la Kibaranga na Shamba la Kibaranga limetengwa kwa ajili ya kilimo cha mkonge tu na mazao mengine ambayo ni ya muda mfupi kama mahindi au alizeti ni sawa kulima ndani ya mkonge.

Alisema Bodi ya Mkonge ndiyo itaratibu ni namna gani ya kuendeleza shamba hilo na eneo na watu wote watazingatia masharti ambayo yatatolewa na Bodi kwenye namna ya uendelezaji wa shamba hilo.

“Sasa watakaochukua hatua za kufanya makubaliano au mauziano huko nje bila kufuata utaratibu ambao utawekwa na Bodi ya Mkonge wasishangae kuona watapoteza hizo ardhi kwa sababu Bodi itawanyang’anya na hatutambui hayo mauziano tutawapa watu ambao wamefuata utaratibu wa kumilikishwa haya mashamba,” alisema.

Alisema bodi inataka watu wajue kilimo cha mkonge ni kilimo makini na kilimo ukikizingatia kitabadilisha hali ya maisha kwa haraka sana.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na Masoko wa Bodi ya Mkonge, Olivo Mtung’e, alisema kwa sasa suala la kujenga makazi ndani ya shamba hilo haliwezekani kwani litaleta mgogoro kutokana na ukweli kwamba baadhi ya watu watauza maeneo yao na baada ya muda mfupi patakuwa makazi ya kudumu.

“Tukisema tujenge huu mgogoro hautakuwa mdogo kwa sababu sisi Waafrika familia zetu huwa zinaongezeka tu ukijenga wewe leo kesho mtoto wako pia atataka kujenga kwa ajili ya makazi, kwa hiyo maana ya kuwa shamba la mkonge itaondoka, kwa hiyo suala la kujenga makazi ya kudumu kwa sasa hapana,”alisema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.