ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 8, 2022

BEI YA MAFUTA YA KULA YAANZA KUSHUKA.

 

CHANZO MWANANCHI

Baada ya machungu ya takriban mwaka mzima ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula nchini, nafuu imeanza kuonekana katika maeneo mbalimbali kwa bidhaa hiyo kuanza kushuka.


Bei zilianza kupanda hata kabla ya kuanza kwa vita ya Ukraine na Urusi Februari mwaka huu kwa dumu la lita 20 kufikia Sh120,000 hadi Sh130,000 kutoka wastani wa Sh55,000 hadi Sh75,000.


Kwa bei za rejareja lita moja ilifikia kati ya Sh8,000 hadi Sh9,000 kutoka Sh5,500 na baadhi ya maeneo yalipanda kutoka Sh6,500.


Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi maeneo mbalimbali umebaini bei ya mafuta imeanza kushuka na kwingine hali ikiendelea kubaki vilevile.


Godfrey James, mfanyabiashara wa duka la rejareja Kinondoni, Dar es Salaam alisema dumu la lita 20 walilokuwa wakinunua Sh115,000 hadi Sh120,000, sasa wananunua kwa Sh92,000 hadi Sh94,000. Alisema lita moja waliyokuwa wakiuza Sh6,500 sasa wanauza Sh5,500 huku Bryan Wambura, mkazi wa Chanika anayeuza kwa bei ya jumla alisema sasa dumu la lita 20 bei yake ni Sh110,000 hadi Sh100,000 kutoka Sh120,000 hadi 130,000 ya awali.


Baby Omar, mkazi wa Buguruni alisema ndoo ndogo iliyokuwa ikiuzwa Sh68,000 mpaka Sh.70,000 sasa inauzwa hadi Sh65,000.


“Hali inaanza kurejea, kwani bidhaa hii ilipanda sana hadi wengine tuliacha kuuza kwa sababu wateja walikuwa hawatuelewi,” alisema Baby.


Vita ya Ukraine imeathiri upandaji wa bei za bidhaa hii kwa sababu kwa mujibu wa ripoti ya Sampuli ya Sensa ya Kitaifa ya Kilimo ya 2019/20 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilionyesha Tanzania ina uwezo wa kuzalisha mafuta yenye kukidhi asilimia 45 ya mahitaji ya mafuta nchini na kiasi kinachobaki huagizwa nje ya nchi.


Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema bei hizo zinashuka kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo jitihada za Serikali kuhamasisha hata wenye viwanda vidogovidogo waongeze uzalishaji.


Alisema katika bajeti hii, Serikali imepunguza hadi asilimia sifuri ya mafuta ghafi ya kupikia kutoka nje, ili kuwawezesha kuyachakata na kuyauza kwa bei nafuu.


Jijini Mwanza, mfanyabishara Peter Maduhu alisema bei ya mafuta ya kula ya alizeti haijapanda wala kushuka na yanaendelea kuuzwa Sh7,000 hadi Sh8,0 00 kwa lita.


Naye, mfanyabishara mkoani Tabora, Jumanne Isack alisema hakuna mabadiliko katika bei ya mafuta huku akisema lita moja ya mafuta ya alizeti inauzwa Sh8,000 na lita tano kati ya Sh32,000 hadi Sh35,000.


Jijini Mbeya bei ya mafuta ya kula katika baadhi ya maeneo imeshuka kutoka Sh7,000 mpaka 5,000 na mama lishe alisema kwa sasa bei ya vyakula imeshuka kutoka Sh 2,500 kwa sahani mpaka Sh2,000 na Sh1,500.


Kwa Kilimanjaro, mfanyabiashara na mzalishaji, Mary Mosha alisema mafuta ya alizeti yamepanda bei kutoka Sh5,500 na sasa yanauzwa Sh6,500 mpaka Sh7,000.


I­­meandikwa na Nasra Abdallah (Dar), Mgongo Kaitira (Mwanza), Hawa Mathias (Mbeya), Ombeni Daniel (Moshi) na Robert Kakwesi (Tabora).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.