ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 25, 2022

BALOZI WA UJERUMANI ATEMBELEA TENDAGURU NA KUSHUHUDIA MFUPA WA MJUSI

 

Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Regine Hess akiwa ameshikilia moja ya mfupa wa mjusi wakubwa wanaopatikana Tendaguru, Lindi alipotembelea eneo hilo Balozi wa Ujeruman nchini Tanzania, Mhe. Regine Hess na mumewe Collins Davidson wakiwa wameshikilia moja ya mfupa wa mjusi mkubwa walioishi eneo la Tendaguru, Lindi miaka zaidi ya miaka milioni 150 iliyopitaBalozi wa Ujeruman nchini Tanzania Mhe. Regine Hess katika picha ya pamoja na wenyeji wa vijiji vinavyozunguka Tendaguru alipotembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki.


Na Mwandishi Wetu, Lindi

Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe.Regine Hess ametembelea eneo la Kipalaentolojia la Tendaguru, Mkoani Lindi ikiwa ni ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo ya Malikale yanayopatikana kusini mwa Tanzania. 

Katika ziara yake kwenye Hifadhi ya Tendaguru, Balozi Hess alifurahishwa na historia ya eneo hilo ambalo masalia ya Mijusi mikubwa aina ya Dinosaria waliopata kuishi takribani miaka milioni 150 iliyopita imekuwa ikipatikana katika eneo hilo. 

Hifadhi hiyo ya Tendaguru ambayo inasimamiwa na Shirika la Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) ni moja ya maeneo muhimu sana Dunia na ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali kuwa Urithi wa Taifa mnamo mwaka 1937. 

Katika ziara hiyo, Mhe. Balozi alishuhudia mfupa ya Masalia ya Mijusi wakubwa takribani kilo 7 hadi 10 na zana za mawe za kati katika eneo hilo la Uhifadhi.

Itakumbukwa ya kwamba kati ya mwaka 1905-1913 takribani tani 225 ya mifupa ya Mijusi ilichimbwa katika eneo hili na kusafirishwa kwenda Ujerumani.

Pamoja na changamoto ya barabara kuelekea katika Hifadhi hiyo, Balozi wa Ujerumani amewapongeza Makumbusho ya Taifa Tanzania (NMT) kwa kazi nzuri ya ujenzi wa kituo cha taarifa eneo la Mkwajuni ambacho kitatoa taarifa juu ya historia ya hifadhi ya Tendaguru pamoja na kuweka maonesho kwa wageni watakaotembelea eneo hilo.

Balozi Hess ambaye pia alipokelewa na viongozi wa vijiji vya Mkwajuni, Mnyangala na Mipingo amepongeza mpango wa Makumbusho ya Taifa Tanzania (NMT) wa kuweka vibao vya maelezo katika hifadhi hiyo ya Tendaguru na kusisitiza juu ya kufanyika kwa utafiti zaidi katika eneo hilo na kuboresha miundombinu kwa ajili ya kupata watalii zaidi katika eneo hilo muhimu kwenye historia ya Dunia. 

Aidha, wakaazi wa maeneo hayo wakiongozwa na viongozi wao, walimuomba Balozi wa Ujerumani kuwasaidia kuboresha miundombinu kwa ajili ya eneo hilo kuweza kufikika kirahisi wakati wote wa majira ya mwaka.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.