ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 7, 2021

KKKT MAMBO BADO SI SHWARI.

 


Hali bado si shwari ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki baada ya aliyekuwa askofu wake, Dk Stephen Munga kumwandikia barua kiongozi wa dayosisi hiyo, Askofu Msafiri Mbilu akipinga tuhuma alizopewa.


Mbali na hilo, Munga pia amewaandikia maaskofu wa kanisa hilo kupinga kuvuliwa uaskofu akiwaeleza kuwa yeye bado ni askofu kwa kuwa uaskofu “hauondoki kihuni, bali kwa kufuata katiba ya dayosisi”.


“Uaskofu haundoki kihuni. Mimi najua taratibu za kuuhifadhi uaskofu. Nimewaarifu maaskofu kwamba sitatekeleza lolote katika barua yao. Tukisema ukweli, (askafu) Mbilu ndio sio askofu kwa sababu amekana katiba iliyomchagua,” ameandika Askofu Munga.


Hata hivyo, Askofu Mbilu alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia suala hilo, alijibu kwa kifupi kuwa hajapata barua ya mtangulizi wake huyo na kwamba, mambo hayo ni ya vikao na asingependa kuyaingiza kwenye magazeti.


Novemba 2 mwaka huu, dayosisi hiyo iliwaandikia barua wachungaji, mashemasi na waamini wote wa dayosisi hiyo, ikiwaeleza maamuzi ya kikao maalumu cha halmashauri kuu ya KKKT kilichokaa Oktoba 29, 2021 Utondolo, Lushoto kumvua uchunguzaji Askofu Munga.


Taarifa hiyo iliyotiwa saini na kaimu katibu mkuu wa dayosisi hiyo, mchungaji Godfrey Walalaze, ilisema kikao hicho kilipitia kwa kina taarifa ya ukaguzi wa hesabu za dayosisi kwa kipindi cha 2019 na 2020 na kumvua uchungaji Dk Munga ambaye ni askofu mstaafu wa dayosisi hiyo.


Halmashauri kuu ilimtuhumu Dk Munga na viongozi wengine kwa kushindwa kusimamia mali za dayosisi wakati wa uongozi wake, kutumia vibaya madaraka kulikosababisha uvunjifu wa katiba na kufanya mambo yanayochochea vurugu.


Hivyo, kwa uamuzi huo Dk Munga aliyekuwa askofu wa dayosisi na mdhamini wa mali, kipindi hicho amevuliwa uchungaji na hivyo kupoteza sifa ya kuwa askofu mstaafu wa dayosisi, huku wachungaji wengine sita waliokuwa chini yake wakisimamishwa nafsi hiyo.


Wachungaji hao ni Dk Eberhadt Ngugi aliyekuwa msaidizi wa askofu, James Mwinuka aliyekuwa katibu mkuu, Dk Aneth Munga aliyekuwa makamu mkuu wa chuo Sekomu na Yambazi Mauya aliyekuwa mkuu wa Jimbo la Tambarare.


Wengine waliosimamishwa uchungaji ni Paulo Diu aliyekuwa mkuu wa Kitengo cha elimu Bombo, Yohana Titu aliyekuwa mlezi wa hospitali ya Bombo na Rodgers Shehumu ambaye hakuwa mchungaji bali, mtunza hazina wa jimbo.


Majibu ya Dk Munga

Katika barua yake kwa Askofu Mbilu Dk Munga anasema uamuzi wa kumvua uchungaji alianza kuutekeleza tangu alipoingia madarakani.


“Tangu Januari 2021 sijapokea posho ya uaskofu mstaafu wala ya mchungaji mstaafu wa dayosisi. Sijaambiwa chochote kuhusu makazi wala usafiri. Ni wazi wewe na viongozi wenzako katika ngazi ya dayosisi na majimbo mmepatana kutowasiliana nami,” alisema.


“Kinachonishangaza ni kuwa hata wachungaji wakija kunisalimu wanatishiwa au kukaripiwa na viongozi wenzako. Haya yote yamekuwa yakiendelea hata kabla ya uamuzi wa halmashauri huu,” anaeleza Munga.


Miongoni mwa anazopinga ni ya kukataa wito wa Tume ya usuluhishi ya KKKT, jambo analosema si la kweli na kuwa ambaye angemtaarifu juu ya uwepo wa Tume ni katibu mkuu wa KKKT.


“(Katibu mku) hajawahi kufanya hivyo. Mkuu wa Kanisa hajanitaarifu juu ya uwepo wa Tume ya jinsi hiyo, wala wewe hujanijulisha. Pili, hakuna chombo cha jinsi hiyo kilichowahi kuundwa kwa ajili ya kuja kusuluhisha mgogoro dayosisini mwetu,” anasema.”


Dk Munga anasema mambo hayo na mengine yanayoendelea, yanadhihirisha kuwa Askofu Mbilu na halmashauri yake wametoa hukumu kabla ya kesi na wamemhukumu kwa tuhuma na si kwa makosa yaliyothibitika.


“Press release (taarifa kwa vyombo vya habari) aliyoandika kaimu katibu mkuu kwa watumishi na washarika wa dayosisi ilisambaa nchi nzima na nje ya nchi kwa lengo la kunichafua ili nisiweze kutokeza uso wangu mahali popote,” anasema.


“Niko tayari kutokea mbele ya Baraza la Maaskofu wa KKKT. Endapo halmashauri kuu ya KKKT itaunda Tume ya usuluhishi kwa mujibu wa taratibu za kanisa, nitakuwa tayari kutoa ushirikiano,” alisisitiza huku akikanusha tuhuma zote.


Katika barua nyingine aliyowaandikia maaskofu wa KKKT, Askofu Munga anasema hawezi kutii agizo dhalimu linalojengwa juu ya mambo ya uongo, hila na chuki.


“Hivyo nitaendelea kuwa askofu aliyestaafu na nitaendelea kutokea kiaskofu pale ninapoona haja ya kufanya hivyo. Askofu Mbilu ameniandikia nisihubiri. Kwa njia ya ubatizo wangu mimi ni mtumishi wa Injili,” anasema.


“Kama ambavyo ubatizo hauwezi kufutika, Askofu Mbilu na halmashauri yake kuu hawana mamlaka ya kunizuia kuhubiri Injili. Kwa msingi wa wito wa uchungaji wangu nitaendelea kuhubiri, kufundisha neno la Mungu na kutoa sakramenti,” anasisitiza.


Katika barua yake hiyo kya kurasa mbili, Dk Munga anahoji kwanini halmashauri kuu ya dayosisi inaongelea kumvua uchungaji wakati mambo wanayoyataja kama sababu yanahusu kipindi cha uaskofu wake.


Alifafanua kuwa mwaka mmoja uliopita, yaani Oktoba 30, 2020, Askofu mstaafu Joseph Jali aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo wakati huo, alisambaza barua kwa wachungaji na kwa baadhi ya washarika akisema amemvua uaskofu.


“Ifahamike kwamba Askofu Jali ni baba mkwe wa Askofu Mbilu. Kwa hiyo ajenda ya kunivua uaskofu ilikuwepo hata kabla ya Dk Mbilu hajawa askofu na sasa anajaribu kuitekeleza,” alidai Askofu Munga katika andiko lake kwa maaskofu.


Askofu Munga amefafanua jinsi uaskofu unavyopatikana, unavyotunzwa na unavyoweza kufika kikomo akisema kuna mambo ya msingi ya kibiblia na ya kikatiba yanayoweza kufikisha ukomo wake nje ya hatua waliyoyochukua


“Barua ya Askofu Mbilu haionyeshi kuzingatia hayo”, anasema Munga na kusisitiza kuwa mambo ya maaskofu humalizwa na Baraza la maaskofu la Kanisa na kwamba hajawahi kuarifiwa kwamba jambo linalomhusu limepelekwa kwenye baraza.


“Hivi sasa mimi ni Askofu mstaafu na ipo misingi ya namna Baraza la Maaskofu linavyoshughulikia maaskofu wastaafu,” alisema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.