Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kesho inatarajiwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwnyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa makossa ya ugaidi.
Hata hivyo masikio ya wadaawa (washtakiwa na mshtaki yaani Jamhuri kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka-DPP) na mawakili wa pande hizo zote, wanafamilia ndugu jamaa na marafiki wa washtakiwa na wadau wengine wanaofuatilia kesi hiyo yatakuwa ni kwenye uamuzi wa mahakama.
Uamuzi huo wa mahakama unaotarajiwa kutolewa kesho Jumatatu Novemba 29, 2021 unahusiana na pingamizi la upande wa mashtaka dhidi ya barua ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohamed Abdillahi Ling’wenya, anayoiomba Mahakama iipokee iwe sehemu ya ushahidi na kilelezo cha ushahidi wa upande wake wa utetezi.
Ling’wenya aliomba mahakama iipokee barua hiyo Ijumaa wakati akitoa ushahidi wake akiwa shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, iliyotokana na maelezo yanayobishaniwa baina yake na upande wa mashtaka.
Upande wa mashtaka unadai kuwa Ling'wenya na mahtakiwa wa pili, Adamu Hassan Kasekwa baada ya kutiwa mbaroni kwa tuhuma za makosa ya ugaidi, walisafirishwa kupelekwa Dar es Salaam.
Wanadai kuwa Dar es Salaam washtakiwa hao walifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, na kwamba walihojiwa na kutoa maelezo yake kituoni hapo.
Wakati upande wa mashtaka ulipoomba kuwasilisha maelezo hayo kupitia kwa shahidi wa nane katika kesi ya msingi, lakini mshtakiwa huyo kupitia kwa Wakili wake Fredrick Kihwelo alipinga kupokewa maelezo hayo wakidai kuwa hakuwahi kufikishwa kituoni hapo wala kutoa maelezo yake kituoni hapo.
Badala yake alidai kuwa Dar es Salaam walifikishwa kituo cha Polisi Tazara na baadaye wakahamishiwa kituo cha Mbweni ambako alipewa nakala ya maelezo na akalazimishwa kuyasaini bila kupewa haki ya kuyasoma huku akitishiwa kupata mateso akikataa.
Kutokana na kupinga maelezo hayo mahakama kama sharia inavyoelekeza, ikalazimika kuendesha kesi ndogo, ili kujiridhisha na madai ya Ling’wenya kama ni ya kweli au la na hatimaye kufikia uamuzi wa kuyapokea au kuyakataa.
Upande wa mashtaka ulilazimika kuwaleta mashahidi kuthibitisha maelezo yake kuwa mshtakiwa huyo na mwenzeka walifikishwa na kuchukuliwa maelezo yake kituoni hapo; akiwemo shahidi wa pili katika hiyo kesi ndogo, Ditektivu Recardo Msemwa.
Pamoja na mambo mengine DC Msemwa alidai kuwa mwaka 2020 alikuwa akifanya kazi Central Dar na kwamba ndiye aliyewapokea Ling'wenya na mwenzake kituoni hapo na kuingiza majina yao kwenye Kitabu cha usajili wa Mahabusu, Agosti 7, 2020, baadaye akahamishiwa kituo cha Polisi Oysterbay.
Lakini Ling’wenya wakati akijitetea kwenye kesi hiyo ndogo, Ijumaa, alisema kuwa baada ya kusikia ushahidi wa shahidi huyo wa pili wa Jamhuri, alimwambia wakili wake, Kihwelo aandike barua kuomba nyaraka za kumthibitisha shahidi huyo kuwa aliwahi kufanya kazi Central, Dar es Salaam.
Hivyo aliiomba mahakama ipokee barua hiyo ya kuomba nyaraka hizo kwa RPC Ilala, lakini upande wa mashtaka ukaipinga, ukidai kuwa shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utete (mshtakiwa wa tatu) hana mamlaka ya kuiwasilisha mahakamani kwani yeye binafsi pamoja na barua yenyewe hajakidhi vigenzo vya kisheria.
Pingamizi hilo liliibua malumbano ya hoja baina ya mawakili wa pande hizo mbili na Jaji Joachim Tiganga anyesikiliza kesi hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo hadi kesho kwa ajili ya uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali.
Msingi wa Ling’wenya na wakili wake kuandika barua hiyo kwa RPC Ilala kuomba nyaraka hizo za uuthibitisho dhidi ya shahidhi huyo wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo ndogo ni kwamba shahidi huyo hakuwa Central Dar es Salaam, mwaka 2020.
Hivyo kama mahakama itatupilia mbali pingamizi la Serikali, na ikaipokea barua yake hiyo basi upande wa mashtaka utakuwa mtegoni.
Maana hatua itakayofuata Ling’wenya ataiomba mahakama hiyo imuamuru RPC Ilala kumpatia au kuwasilisha mahakamani hapo nyaraka hizo alizoziomba ili kujiridhisha kama kweli mwaka 2020 DC Msemwa alikuwa akifanya kazi Central.
Lakini kama nyaraka hizo zisipopatikana au kuletwa na zisiwe na uthibitisho huo, ni dhahiri ushahidi wa shahidi huyo wa pili wa upande wa mashtaka hautakuwa na miguu ya kusimamia.
Mbali na Mbowe (ambaye ni mshtakiwa wa nne), Kasekwa (wa pili) na , Ling’wenya mwenyewe (wa tatu) mshtakiwa mwinginen ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza)
Wote wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita, ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kushiriki na kufadhili vitendo vya kigaidi, kutaka kulipua vituo vya mafuta, kuhamaisha maandamano yasiyokoma kukata miti na kuiweka barabarani kuzuia barana na kutaka kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.