ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, February 11, 2020

Huduma ya Fahari Kilimo ni mkombozi kwa wakulima wa Pamba- RC Mtaka

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungumza kwenye Kongamano la Wadau wa Sekta ya Kilimo lililoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Shirika la Uwezeshaji Sekta ya Kilimo (PASS).
Mkurugenzi wa Mikopo Benki ya CRDB, Xavery Makwi akizungumza kwenye kongamano hilo.
Meneja wa Kanda ya Ziwa Benki ya CRDB, Lusingi Sitta akielezea fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB ikiwemo mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima wa Pamba.
Mmoja wa wadau wa zao la Pamba akichangia mada wakati wa Kongamano hilo.
Mmoja wa wadau wa zao la Pamba akichangia mada wakati wa Kongamano hilo. 
Mkurugenzi wa kampuni ya uchenjuaji Pamba Nsagali Ltd, Gungu Silanga akielezea namna ambavyo kampuni hiyo imenufaika na mikopo ya uwezeshaji kwa viwanda inayotolewa na Benki ya CRDB. 
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akitoa salamu zake wakati wa kongamano hilo.
Afisa Kilimo wa Wilaya ya Bariadi, Golang'a Ally akitoa taarifa kuhusu kilimo cha Pamba katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akichangia hoja wakati wa kongamano hilo.
Wakulima wa zao la Pamba wakiendelea na zoezi la kujaza fomu kwa ajili ya kufungua akaunti CRDB.
Wakulima wakijisajili ili kumiliki akaunti CRDB.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Wadau wa kilimo wakifuatilia kongamano hilo. 
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema akaunti ya Fahari Kilimo kupitia Benki ya CRDB imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa Pamba kanda ya ziwa. Mtaka amesema huduma zinazoambatana na akaunti ya Fahari Kilimo ikiwemo mikopo ya pembejeo na zana za kilimo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija kwa wakulima pamoja na kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini. 

Mtaka aliyasema hayo Februari 10, 2020 wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya kilimo lilioandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Shirika la Uwezeshaji Sekta ya Kilimo (PASS). Akitoa hotuba yake katika kongamano hilo ambalo lilihusisha mikoa ya Simiyu, Mwanza na Mara, Mtaka aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha Pamba. 

"Sote tunafahamu changamoto ambayo tuliipata katika zao la Pamba mwaka jana, lakini Benki ya CRDB ilionyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kushirikiana na Serikali kutoa mikopo kwa wanunuzi wa Pamba lakini pia kutafuta masoko ndani na nje ya nchi, hili ni jambo la kupongezwa sana" alisema Mtaka. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uendelezaji zao lao la Pamba, Adam Malima alisema Serikali inaridhishwa na jitihada kubwa zinazofanywa na Benki hii ya CRDB katika kuboresha sekta ya kilimo nchini. Malima alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejidhatiti katika kuhakikisha zao la Pamba linaongezeka thamani ili kuboresha maisha ya wakulima wa Pamba.

"Niwaombe wakulima wetu wa Pamba tuendelee kutumia fursa hizi zinazotolewa na Benki yetu ya CRDB, tukifanya hivyo tutaweza kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya kilimo chetu. Serikali ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Benki ya CRDB kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea" alisema Mtaka. 

Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi alisema akaunti ya Fahari Kilimo ni sehemu ya mkakati mpana wa benki kuwahudumia wakulima kwa ukaribu zaidi kwa kuzingatia mahitaji yao. Makwi alisema mpaka sasa wakulima zaidi ya 30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya FahariKilimo na hivyo kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB. 

"Akaunti hii ya FahariKilimo hufunguliwa bure kabisa na hakuna gharama zozote za uendeshaji wa akaunti kwa mkulima, tukilenga kumpa mkulima unafuu wa kupokea malipo yake pindi anapopokea malipo baada ya kuuza mazao" alisema Makwi. 

Makwi alisema wakulima ambao wamejiunga na Fahari Kilimo wameweza kunufaika na mikopo ya pembejeo, mikopo ya zana za kilimo, mikopo ya ujenzi wa maghala, pamoja na uunganishwaji na masoko. "Uwezeshaji huu tunaufanya pia katika uwekezaji katika viwanda vya uchenjuaji Pamba" alisema Makwi.

Makwi alisema baadhi ya viwanda vilivyonufaika na uwezeshaji huu unaofanywa na Benki ya CRDB ni pamoja na Gaki Investment Company Ltd, Fresho Investment Company Ltd, Aham Investment Company Ltd, Nsagali Company Ltd na Birchand Oil Mill Limited. 

Naye Meneja wa PASS Kanda ya Ziwa, Langelika Kalebi alisema shirik a hilo litaendelea kushirikiana na Benki ya CRDB kuwawezesha wakulima na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) wa Pamba hususani katika kuandaa mpango wa kilimo na uongezaji wa thamani wa dhamana ikiwa ni vitu muhimu vinavyohitajika wakati wa uombaji wa mikopo ya pembejeo, zana za kilimo na maghala. 

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Pamba, Medard Marko ambaye ni mkulima wa Pamba kutoka Bariadi vijijini aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mkombozi kwa wakulima kupitia akaunti ya Fahari Kilimo. "Kupitia akaunti hii tumekuwa tukipata mafunzo ya mara kwa mara juu ya uboreshwaji wa kilimo chetu, lakini pia tumekuwa tukiunganishwa na huduma za mikopo ya pembejeo, zana za kilimo kama matrekta na ujenzi wa maghala kupitia AMCOS" alisema Marko. 

Takwimu zinaonyesha Mkoa wa Simiyu unaongoza nchini kwa uzalishaji wa zao la Pamba, akizungumza katika kongamano hilo Afisa Kilimo wa Wilaya ya Bariadi, Golong’a Ally alisema mwaka jana Mkoa huo ulizalisha zaidi ya kilo milioni 160 za Pamba. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.