ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 4, 2020

KUTOPANDA MADARAJA KWA WALIMU TATIZO LINASABABISHWA NA BAADHI YA MAAFISAUTUMISHI WENYE ROHO ZA NYOKA



KATIKA kuwatoa shaka waalimu kuhusu malalamiko yao ya kutopanda madaraja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemeni Jafo ametoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha walimu wanaostahili kupanda madaraja wanapandishwa madaraja. Waziri Jafo ametoa kauli hiyo katika Tamasha la utoaji TUZO ZA UMAHIRI KATIKA ELIMU MKOA WA MWANZA zilizoanzishwa na wadau wa elimu mkoa huo kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha na kuongeza kiwango cha ufaulu kimkoa. "Daraja halipandishwi na Magufuli, hapandishi Mama Samia wala Majaliwa, wala Jafo, mchakato wa madaraja unaanzia kwenu wenyewe, iweje leo Afisa Utumishi katika Halmashauri fulani anashindwa kuweka katika bajeti yake ya makisio ya Mwaka, kwamaba watumishi fulani watapanda madaraja?" Alihoji Waziri Jafo na kuongeza..... "Wewe Afisa Utumishi leo hii watu wamepewa barua ya kupanda daraja lakini kwenye makisio ya mshahara mtu hayupo, halafu tunahamisha lawama kusema Serikali imeshindwa kupandisha watu madaraja, kumbe kuna watu tunaokaa nao wanaroho kama za nyoka. Ni matatizo ya baadhi ya Maafisa Utumishi wanaoshindwa kupanga utaratibu wa watu kupanda madaraja kutokana na sababu zao binafsi" Halmashauri ya Jiji la Mwanza imekuja na wazo hilo ili kufikia malengo yake iliyojiwekea kwa Shule zake kwa miaka ijayo kuongoza katika chati ya ufaulu kitaifa. Ikumbukwe kwamba Halmashauri ya Jiji la Mwanza/Wilaya ya Nyamagana imekuwa Mshindi wa pili Kimkoa kwa matokeo ya Elimu Msingi Darasa la Saba Mwaka 2019-2020, Ya Nne katika matokeo Kitaifa huku shule zake mbili za Serikali zikiwa ndani ya Kumi Bora na baadhi ya Shule zake binafsi zikiwa ndani ya Tano Bora. Kwa matokeo hayo Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeona ipo sababu ya kutia hamasa kwa Waalimu na watendaji Sekta ya Elimu, kusherehekea na kutoa tuzo kwa wanafunzi na shule zilizo ongoza sanjari na kuweka mkakati kuhakikisha Halmashauri hiyo inakuwa ya kwanza kwenye matokeo yajayo. Tuzo za Elimu Mkoa wa Mwanza zinaratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza Ofisi ya Mbunge na Wadau mbalimbali wa Taasisi za Kifedha, Watu, Mashirika Binafsi na Wafanya Biashara waliojitokeza kuweka chachu katika zawadi na udhamini. KAULI MBIU INAYOSHIKA MKAKATI HUO NI 'MWANZA KUWA WA KWANZA INAWEZEKANA'

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.