ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, January 6, 2020

KIVUKO KIPYA CHA MV ILEMELA CHASHUSHWA ZIWA VICTORIA KWA MARA YA KWANZA.


TANGU dunia kuumbwa hata nchi yetu kupata Uhuru Wananchi wa Kisiwa cha Bezi mkoani Mwanza hawajawahi kuwa na kivuko au usafiri wa uhakika wa meli zaidi ya kutumia mitumbwi na boti ndogo kusafiri na kusafirisha mizigo yao kusaka huduma muhimu toka maeneo tofautitofauti hali ambayo imesababisha mara kadhaa wananchi hao wasafiri kukumbwa na madhila mbalimbali yaliyoletwa na ajali.

Hatimaye Leo tarehe 6 mwezi Januari 2020 Ahadi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula ya kutatua kero ya usafiri wa uhakika kwa wananchi wa visiwa hivyo aliyoitoa kipindi cha uchaguzi mkuu 2015 imetimia baada ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kujenga kivuko chenye uwezo wa kubeba abiria 200, tani 10 za mizigo na magari 10 na kukiingiza majini ziwani Victoria tayari kuanza kutoa huduma ya usafiri. 

 Akizungumza na wananchi hao wakati wa kukiingiza kivuko hicho katika ziwa Victoria, Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditie amesema kivuko hicho kimejengwa baada ya wananchi kuwasilisha vilio vyao.

Mradi huo umetekelezwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano chini ya usimamizi wa Wakala wa Ufundi na Umeme TAMESA baada ya kampuni ya ujenzi na utengenezaji meli ya Songora Marine kushinda zabuni ya utengenezaji wa kivuko hicho.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Angeline Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kituo hicho kitafuta machozi ya wananchi huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella akiipongeza Serikali kwa ukamilishaji wa ujenzi wa kivuko hicho.

Kukamilika kwa kivuko hicho kunakwenda sambamba  na ujenzi wa vivuko vingine viwili vya Mv Chato na Mv Ukara vinavyotarajiwa kukamilika Februari Mwaka huu ili kuanza kuhudumia wananchi.











 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni iliyotengeneza kivuko hicho ya Songoro Marine Ltd ya jijini Mwanza, Meja Songoro ameishukuru Serikali kwa kuiamini kampuni yake na kuikabidhi tenda kadhaa ikiwemo ya ujenzi wa meli hiyo na nyinginezo nchini kwani kwa mfumo huo, serikali inazidi kuvijengea uwezo viwanda vyake vya ndani.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa kwa mgeni rasmi katika tukio hilo alisema serikali kupitia TEMESA inaendelea na ujenzi wa vivuko vingine vipya kwa ajili ya Mafia Nyamisati kwa gharama ya shilingi bilioni 5.3, Bugorola Ukara kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 pamoja na Chato Nkome kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1.


Ujenzi wa kivuko cha Mv Ilemela umegharimu kiasi cha bilioni 2.7. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.