ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, January 27, 2020

Bunge lanusa ufisadi wa bilioni 15 Machinjio ya Dodoma, laagiza vigogo NARCO, NICOL wakamatwe


Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeagiza kukamatwa na kushtakiwa  Watendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Watendaji Wakuu wa Wizara ya Mifugo pamoja na Viongozi wa Kampuni ya Taifa ya uwekezaji (NICOL) kufuatia kashfa ya uchotwaji wa Shilingi bilioni 15 kwenye Biashara ya Uendeshaji wa Machinjio ya Dodoma katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa alisema watendaji wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliohudumu katika  kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2015 ambapo walishirikiana kwa pamoja na Kampuni ya NICOL kuwaibia watanzania fedha hizo jambo ambalo Bunge 11 kamwe haliwezi kubariki wizi huo mkubwa wa fedha za watanzania.

Akizungumza kwenye ziara ya kamati hiyo kutembelea machinjio ya Dodoma ambayo kwa sasa inaendeshwa Serikali baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuvunja mkataba huo mbovu baina ya NARCO na NICOL  uliooingiizia hasara Serikali kwa kipindi cha miaka 11 huku wahusika waliohusika na kashfa hiyo wakiwa bado hawajachukuliwa hatua yoyote.

Mgimwa alielezwa kushangazwa na usimamizi mbovu, ubadhirifu na ukiukwaji mkubwa wa mkataba uendeshaji wa machinjio hiyo na kuelezea kusikitishwa kwake na watendaji  waliopewa dhamana kusimamia mali hiyo kwa niaba ya watanzania kushirikiana kufanya hujuma hiyo.

Mgimwa alihoji iweje tangu mwaka 2008 ufisadi huo umefanyika bila wahusika kuchukulia hatua wakiwemo waliokuwa watendaji wa NARCO, NICOL na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwatafuta na kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria.

Pia Kamati hiyo imepongeza uamuzi wa Serikali ya kuvunja mkataba wa mauzo ya mali za machinjio ya Dodoma baina ya Serikali na Kampuni ya NICOL na kuirejesha machinjio hiyo chini ya umiliki wa Serikali na kuitaka kufanya haraka kurejesha masoko ya nyama katika nchi za Falme za Kiarabu yaliyopotea kutokana na usimamizi mbovu wa waendeshaji hao wa zamani.

Pia Kamati imeitaka Serikali kuhakikisha fedha zote kiasi cha jumla ya shilingi 9,712,127,660 ambazo Serikali ilimeibiwa katika biashara ya machinjio zinalipwa haraka pamoja mbia NICOL kulipa madeni yote inayodaiwa Kampuni ya Ubia TMCL kiasi cha shilingi 5,248,084,000.

Mbali na Kamati hiyo kupongeza uamuzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambaye ni mbia katika Kampuni ya Ubia TMCL kujiondoa kwenye ubia wa Kampuni ya TMCL bado viongozi waliohusika na ufisadi huo waweze kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Antony Komu alisema uamuzi uliofanywa na Waziri Mpina katika kubaini kasoro hizo na kuchukua hatua unapaswa kuendelezwa kwa Serikali kutengeneza mfumo endelevu wa kubaini udhaifu na kuchukua hatua kwani ni jambo la kusikitisha kuona  ufisadi mkubwa kiasi hicho umefanyika bila ya wahusika kuchukuliwa hatua.

Komu alitaka hatua kama hizo ziwe endelevu ili kunusuru mali za nchi badala ya kumuachia kiongozi  mmoja tu ambaye ni Waziri Mpina kusimamia mambo kama hayo.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali iko kwenye hatua ya mwisho ya kuifanyia ukarabati mkubwa machinjio hiyo na kurejesha upya masoko ya nyama nje ya nchi ikiwemo nchi za Famle ya Kiarabu na Comoro.

Pia ameihakikishia kamati hiyo kuwa wote waliohusika na wizi na ubadhirifu hawatapona kwani Serikali inajua kuwa mbali na fedha hizo zilizoibwa za watanzania bado hata mishahara ya wafanyakazi wa kampuni hiyo nayo ilifanyiwa ufisadi na kuleta usumbufu mkubwa watumishi.

Waziri Mpina alisema kwa muda mrefu Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kurekebisha kasoro za uendeshaji wa Machinjio ya Dodoma kama sharti muhimu katika Mkataba wa Mauzo ya Mali kwenye Ibara ya 4.1.3.1 na kwa kuwa jitihada za kuinusuru Machinjio hiyo zimefanyika kwa muda mrefu bila ya mafanikio yoyote.

Hivyo Serikali ilijiridhisha kwamba Mbia (NICOL) amekiuka vipengele muhimu vya Mkataba katika Ibara ya 7, 13, 6, 9 na 102; Pia NICOL imekuwa ikifanya biashara na mali za Kampuni bila ya kuwekeza na bila ya kutoa gawio kwa Serikali kwa kipindi chote cha miaka 11 alichokabidhiwa Kiwanda hicho;

Waziri Mpina amesema tangu machinjio hiyo ibinafsishwe Serikali imeendelea kupata hasara na mali nyingi za Kampuni kama mitambo, majengo, magari na rasilimali nyingine zimechakaa na hakuna ukarabati wowote uliofanyika;

Pia nchi yetu imepoteza ajira, fedha za kigeni, biashara na masoko ya mazao ya mifugo baada ya Kiwanda kufungiwa kuuza mazao ya mifugo katika nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE).

Aidha, Kampuni 10 zilisimama kusafirisha na kufanya biashara ya nyama baada ya Kiwanda kufungiwa ambapo kwa mwezi mauzo ya nyama nje ya nchi katika Machinjio yalikuwa yamefikia tani 192 sawa na mbuzi 24,000 kwa mwezi. Pia, kiwango cha uchinjaji wa ng’ombe kushuka kutoka wastani wa ng’ombe 120 hadi 50 kwa siku;

Hata hivyo hasara na madeni ya Kiwanda cha TMCL yanaendelea kukua kila uchao huku Mbia (NICOL) akishindwa kurekebisha kasoro zilizobainika katika vipindi tofauti hata baada ya kupewa notisi ya muda wa siku 30 na hata Mbia mwenzake (NARCO) kumpa notisi ya siku 180, pia, ziara za Viongozi katika Machinjio akiwemo Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.