ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 31, 2019

TANZANIA: MAMA WA MWANDISHI WA HABARI ERICK KABENDERA AFARIKI.

Mama mzazi wa mwandishi wa habari Erick KabenderaMama wa mwandishi wa habari aliye mahabusu nchini Tanzania Erick Kabendera amefariki dunia, familia imethibitisha.

CHANZO:- BBC Swahili.
Bi Verdiana Mjwahuzi (81) amefikwa na umauti katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumanne.
Alipelekwa hospitalini hapo siku ya Jumamosi wakati hali yake ikiwa mbaya. Hata hivyo kufikia mapema jana taarifa zilisema hali yake ilikuwa ikiendelea kuimarika.
Kabendera yupo rumande akikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi.
Hivi karibuni mama Verdiana Mjwahuzi (81) alimuomba Rais John Magufuli kumsamehe mwanae.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bi Verdiana alisema mwanae Kabendera ni nguzo muhimu ya ustawi wa familia yake.
"Mheshimiwa Rais na yeye ni mtoto kama walivyo watoto wengine hata kama ni mkubwa. Ni mzazi na analea watoto. Namwomba anionee huruma. Angalia maisha yalivyo magumu, dawa sipati. Naomba Rais anisaidie kama anavyosaidia wazazi wake," alisema Bi Verdiana.

Mwandishi Erick Kabendera
Erick Kabendera alikamatwa mwezi Julai 2019 na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, kukwepa kodi na kuongoza kikundi cha uhalifu. Mashtaka ambayo mawakili wake wameyakana.
Tayari mawakili wake wamefungua majadiliano na mkurugenzi wa mashtaka wa serikali (DPP) kukiri makosa na kuomba msamaha.
Wakati Kabendera anakamatwa, tayari afya ya mama yake ilikuwa dhoofu.

Kabendera ni mtoto wa saba kuzaliwa kati ya watoto nane wa Bi Verdiana.
Alisema pamoja na kuwa mdogo kati ya wanae, Kabendera ni mtoto ambaye mara tu anaposikia mama yake anaumwa hukimbia mara moja aidha kumpatia matibabu au kwenda kumuona nyumbani kwake.
"Huyu mtoto ni Mungu amenizawadia, ni tunu kwangu. Akisikia mama anaumwa anakimbia haraka. Sasa hizo dawa sizipati tena, macho yalikuwa yanauma na moja halioni tena na hili linaloona naona vitu vyeusi," alisema Bi Verdiana.
Alimuelezea mwanae kwamba hana hulka ya kusema watu vibaya, asiyependa anasa na mchapa kazi. Bi Verdiana ana amini kwamba mashtaka dhidi ya Kabendera yanatokana na kazi zake za uandishi wa habari.

Bi.Verdiana

"Siwezi kumsifia mwanangu, wanaume wengi wakitoka kazini wanakwenda kulewa lakini Eric anafanya kazi zake hapa nyumbani hadi saa saba usiku na wakati mwingine hadi saa nane . Mambo yote aliyopata ni kwa sababu ya kufanya kazi," alisema Bi Verdiana huku akibubujikwa machozi.
Bi Verdiana pia alieleza masikitiko yake ya kushindwa kwenda kumsalimia mwanae aliyeko rumande.
"Kule Segerea (gerezani) siwezi kwenda kwa sababu kuna msongamano wa watu, mahakamani kuna ngazi. Lakini mara ya mwisho nilijitahidi nikaenda nilipomuona mwanangu sikulia, nilijikaza lakini chozi moja lilinitoka. Sikujua kama ni yeye, amekonda na ana nywele nyingi kama mwehu. Ni mweusi lakini amezidi kuwa mweusi," alisema Bi Verdiana kwa uhuzuni. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.