Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Moshi, nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu Askofu Ludovick Joseph Minde alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki Kahama. Itakumbukwa kwamba, Askofu Minde alizaliwa tarehe 9 Desemba 1952 kwenye Parokia ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi.
Ni mtoto wa mzee Joseph Ndasika Minde na Mama Maria Joseph Mukure. Baada ya masomo yake Seminari Ndogo ya Mtakatifu James, Jimbo Katoliki la Moshi kunako mwaka 1979 alijiunga na Shirika la Mapadre wa Maisha ya Kitume na Kazi ya Roho Mtakatifu ALCP/OSS. Akaendelea na masomo yake ya falsafa Seminari kuu ya Kibosho na kuhitimisha masomo ya taalimungu kwenye Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Tarehe 26 Juni 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 24 Aprili 2001 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 5 Agosti 2001 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Askofu Mathew Shija, Muasisi wa Jimbo Katoliki la Kahama pamoja na Hayati Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi.
Itakumbukwa kwamba, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ni kati ya Mapadre watano walioteuliwa kwenda Roma kwa masomo zaidi baada ya hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania kunako mwaka 1990. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuimarisha malezi na makuzi ya majandokasisi kutoka Tanzania.
Tangu mwaka 1990 hadi mwaka 1995 alikuwa mjini Roma akijifunza Maandiko Matakatifu na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Ni kati ya wanafunzi waliofanya vizuri sana katika masomo yao kwa mwaka huo.
Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Jaalimu wa Maandiko Matakatifu, Mlezi na Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Itakumbukwa kwamba, Jimbo katoliki la Moshi limekuwa wazi baada ya Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Desemba 2017 kumteua Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Kuu la Arusha, nchini Tanzania.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.