Nteghenjwa Hosseah OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewatunuku wanafunzi 4191 tuzo za Astashahada ya awali, kati na Stashahada za chuo cha Serikali za Mitaa mapema leo Tarehe 31/10/2019 katika viwanja vya Magufuli Square vilivyopo Hombolo chuoni hapo.
Akiwa katika Mahafali hiyo Waziri Jafo amewataka wanafunzi hao kwenda kufanya kazi kwa weledi na uaminifu ili waweze kutangaza sifa njema ya Chuo cha Serikali za Mitaa.
“Najua wengi hapa mtaajiriwa na mtaajiriwa katika Halmashauri zetu nataka muende mkazitendee haki halmashauri hizo, mkafanye kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya katika mamlaka zetu za Serikali za Mitaa”
Chuo hiki kinatoa maarifa stahiki kwa mahitaji ya soko la ajira la sasa, napokea sifa nyingi za wahitimu wa chuo hiki wanapofanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini, naamini ninyi mnaohitumu leo mmeiva vyema kwenda kulitumika Taifa hili alisema Jafo.
Aliongeza kuwa Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma ukawe muongozo wenu katika utendaji kazi wenu wa kila siku, mkafanye kazi kwa umakini mkubwa ili tuzidi kuwa na wataalamu wenye weledi ili maendeleo ya Taifa yaweze kufikiwa.
Wakati huo huo Waziri Jafo amezitaka Halmashauri zote kuanza kutumia mfumo ulioboreshwa wa fursa na vikwanzo kwa maendeleo ambao umeandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kwa kushirikiana na JICA.
“Mfumo huu ulioboreshwa utazisaidia Halmashauri zetu katika kupambana na vikwanzo vya maendeleo na kuona ni namna gani zinaweza kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo hayo” Alisema Jafo.
Nikipongeze chuo hiki kwa kuwa wabobezi na mahiri katika maandiko yenye kutoa Dira na muelekeo wa kupambana na changamoto zilizoko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa alimalizia Jafo.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Mpamila Madale amesema chuo hicho mbali na kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi pia wamejikita katika Tafiti, kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kuandaa machapisho ya kitaaluma.
Alisema mpaka sasa chuo cha Serikali za Mitaa kina jumla ya wanafunzi 7436 na ongezeko la wanafunzi hao kumepelekea uhaba wa madarasa ambapo kwa mwaka huu wameweza kujenga darasa moja lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 504 kwa kutumia mapato ya ndani na ujenzi huo umetumia force account.
Mahafali haya ni mahafali ya kumi na moja na yamehudhurisha wahitimu wa Astashahada ya awali ya ugavi na manunuzi, menejiment ya rasilimali watu,utunzaji wa kumbukumbu, pamoja na maendeleo ya jamii.
Wanafunzi walohitimu kwenye Astashahada ya kati ni Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha katika Serikali za Mitaa, Ugavi na manunuzi,menejiment ya rasilimali watu, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na Astashahada ya kati ya maendeleo ya jamii;
Wakati huo huo wanaofunzi waliohitimu katika ngazi ya Shahada ni Utawala katika Serikali za Mitaa, Uhasibu na Fedha katika Serikali za Mitaa, Menejiment ya Rasilimali watu, Maendeleo ya jamii, Ugavi na manunuzi pamoja na Stashahada ya Utunzaji wa Kumbukumbu 2019.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.