Kaimu Katibu Mkuu akizungumza katika kikaokazi cha Wakurugenzi wapya.
Zoezi la kiapo cha uadilifu likiendelea.
Picha ya pamoja mara baada ya Hotuba ya Mhe. Waziri wakati wakikaokazi hicho.
Kiapo kikiendelea.
‘Wakurugenzi Msiingie Mtegoni’ – Jafo
Na. Atley Kuni- TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Seleman Jafo amewatahadharisha wakurugenzi wapya walioteuliwa hivi karibuni kukwepa mtego uliowanasa wenzao waliondolewa madarakani na badala yake wakajenge mshikamano na umoja kwa watumishi watakao wakuta kwenye vituo vyao vipya vya kazi.
Akizungumza katika kikaokazi cha Wakurugenzi hao kilichokwenda sambamba na zoezi la kula kiapo cha Maadili kwa viongozi wa umma, Jafo amewatahadharisha viongozi hao dhidi ya baadhi ya watumishi watakao wapelekea majungu kwakujipendekeza na kutaka kuchonganisha watendaji na kuvuruga utendaji wa Halmashauri.
“Ajenda kuu ya Serikali hivi sasa ni ukusanyaji wa mapato, lakini pia usimamizi wa Miradi ya maendeleo ikiwepo fedha za vituo vya afya ambazo baadhi walishindwa kuzisimamia hivyo ili muweze kufanikiwa katika hili lazima mkatengeneze mahusiano na morali miongoni mwa watumishi ili msikwame na watu wachape kazi kwa hamasa kubwa” alisema Waziri Jafo.
Awali akitoa maneno ya utangulizi, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mathias Kabunduguru, aliwataka wakurugenzi hao watambue huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivyo wakasimamie ipasavyo zoezi la kuandikisha wapiga kura litakalo anza tarehe 08 Oktoba, 2019.
“Idadi kubwa mlioteuliwa mlikuwa watumishi katika ngazi ya mamlaka ya Serikali za Mitaa, hivyo haitakuwa kazi sana, lakini yapo yale ambayo yalikuwa yanakukera ukiwa kama Afisa Tarafa unapoagizwa na Mkurugenzi, sasa hayo usiende kuwafanyia waliochini yako bali mkafanye kazi kwa ushirikiano” Alisema Kabunduguru.
Bw. Mohamed Mavura ni miongoni mwa Wakurugenzi wapya aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, amesema kuwa anakwenda Kibiti akiwa anajua kabisa ipo Miradi ya Maendeleo, suala la mapato, lakini pia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hivyo ameahidi kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama Waziri alivyowaasa.
Wakurugenzi waliokula kiapo hicho mbele ya Afisa Mfawidhi wa Sekretarieti ya Maadili ni pamoja na Bw. Ndaki Stephano Muhuli, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Bi. Rehema Said Bwasi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Sheillah Edward Lukuba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro, Bw. Mohamed Mavura Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Wengine ni Bw. Ezekiel Henrick Magehema, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Bi. Diana Sono Zacharia, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Bi. Hanji Godigodi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Said H. Magaro Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Bi. Hawa Lumuli Mposi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, na Bw. Godwin Justin Chacha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.