ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, September 9, 2019

'CCM SI CHAMA CHA UCHAGUZI BALI CHA KUHANGAIKA NA MAENDELEO YA WATU'



NA BALTAZAR MASHAKA, MISUNGWI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kimesema si Chama cha uchaguzi, kinahangaika na maendeleo ya wananchi na hata wasiokipigia kura wanayahitaji hivyo  Makatibu wa Kata na Matawi wajipange kupata wagombea wanaoguswa na maendeleo .

Pia wahakikishe wanazingatia mabadiliko ya Katiba ya CCM na kanuni  zake pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwaeleza wananchi mazuri yaliyofanywa  na serikali  ya CCM, kufanya hivyo wataisaidia kuibuka na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Hayo yalielezwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza,Salum Kalli, alipozungumza na makatibu hao wa kata na matawi wa tarafa za Misasi na Mbarika, katika Wilaya  Misungwi jana akisema CCM si chama cha kusubiri uchaguzi bali kinahangaika na maendeleo ya wananchi na kujenga uchumi.

Alisema mabadiliko makubwa ya Katiba ya CCM yaliyofanywa mwaka 2017 na kanuni zake yaliathiri mambo mengi na hivyo kipimo na majaribio yake yatafanyika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani ili kurejesha vijiji na vitongoji vilivyoangukia kwa wapinzani wilayani Misungwi.

Alisema makatibu wa kata na matawi waielewe katiba na kanuni katika mchakato wa kupitisha wagombea,wajipange kupata  wagombea wenye sifa wanaotokana na CCM wasio na makunyanzi, wanaokubalika ambao itakuwa rahisi kuwanadi na si kupitisha wagombea mizigo.

“Kwenye uchaguzi huu tujiongeze tusije kuletewa wagombea mizigo ya ajabu bali wanaokubalika kwa sifa zao, viongozi waliochokwa na wananchi wasirejeshwe kuwania nafasi yoyote vinginevyo itakuwa tatizo.Pia watafutwe mameneja kampeni watakaoeleza kazi zilizotekelezwa na serikali ya CCM maana viongozi tunaowatafuta  wengine hawajui lolote kwenye ilani,”alisema Kalli.

Alisema kuwa siasa ni sayansi na ushindi kwenye uchaguzi ni namba na kutahadharisha kuwa licha ya  Rais John Magufuli kufanya mengi mazuri mengine nje ya ilani unaweza kushangaa kwa sababu tu imekosekana tafsiri ya yaliyofanyika, hivyo wananchi wakumbushwe hayo ili kuongeza mtaji wa kura.

Aidha, Kalli alieleza kuwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa ajabu ajabu wasipitishwe ambao wananchi na wana CCM hawajawahi kuwaona, hivyo vikao vya uteuzi vizingatie haki kwa sababu Rais Magufuli ana mambo mengi ya kujenga uchumi wan chi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Aliongeza kuwa yapo mambo watendaji wa Chama hawayafanyi ya kutatua kero za wananchi na wala hawaishi na matatizo yao, hivyo akawataka wakaishi na shida za wananchi,wakatatue kero na migogoro na wakiyafanya hayo na kutimiza wajibu wao CCM itakuwa kimbilio la wanyonge watakuwa wanamsaidia Rais.

Pia katibu huyo wa CCM Mkoa wa Mwanza alikemea makundi ya uchaguzi na kuhimiza uhusiano baina ya watendaji wa Chama na watumishi wa serikali kuhakikisha ilani ya uchaguzi imetekelezwa na wananchi kupata mrejesho wa shughuli na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali yao.

Picha
Katibu wa CCM MKoa wa Mwanza, salum Kalli akizungumza na makatibu wa kata na matawi wa kata za Mbarika na Misiasi wilayani Misungwi (hawapo pichani).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.