SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetinga jijini Mwanza tayari kufanya uhakiki wa mgongano wa kimasilahi wa viongozi wa umma.
Lengo la uhakiki huo ni kuangalia taarifa za mali na madeni kupitia tamko la rasilimali na madeni walizojaza viongozi hao, wenza wao pamoja na watoto wao walio chini ya miaka 18 kama zinawiana.
Jaji Nsekela amesema shughuli hiyo ni ya kawaida kwa sababu sekretarieti ilianzishwa ili kusimamia mienendo na tabia za viongozi wa umma pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 pamoja na marekebisho yake.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni muendelezo wa uhakiki unaoendelea nchini ambapo umelenga viongozi 600 walioko kwenye mikoa 12 hapa nchini.
Mbali na Mwanza mikoa mingine iliyolengwa na uhakiki huo ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Geita, Kagera, Mara, Dodoma, Tabora, Singida, Dar es Salaam na Shinyanga.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa viongozi hao 600 wanaohusika na uhakiki huo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini wa taasisi hiyo, Honoratus Ishengoma alisema, “sheria yetu ukiiangalia vizuri kifungu cha 4 kinataja aina ya viongozi tunaowasimamia kutoka mihimili yote mitatu. Aina za viongozi wanaohakikiwa wanatokana na mihimili hiyo.”
Ingawa Ishengoma hakutaka kuwataka moja kwa moja majina yao baadhi yao ni; madiwani, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, mahakimu pamoja na majaji.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.