ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 29, 2019

MSIDANGANYIKE, HAKUNA MBADALA WA ARV - TACAIDS


Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imewataka watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutodanganyika na kuacha kutumia dawa kupunguza makali ya VVU kwani hakuna mbadala wa ARV.


Rai hiyo imetolewa  na Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango wakati akifunga Kambi ya Ariel 2019 iliyoandaliwa na asasi inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI).

Akizungumza kwenye kambi hiyo iliyojumuisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Mara Bw. Issango alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa watu wengine wanaacha kutumia ARV na kisha kujikita kwenye dawa za kienyeji au maombi. “Matokeo yake ni VVU kuendelea kuwashambulia. Kinachosaidia kupunguza makali ya VVU mwilini ni ARV peke yake, hakuna mbadala,” alisisitiza.

Mkurugenzi huyo alisema, “Msidanganyike mkaacha kutumia dawa za ARV, mpaka sasa bado wanasayansi hawajapata dawa nyingine. Tunaamini ipo siku dawa itapatikana lakini kwa sasa wenye maambukizi ya VVU endeleeni kuwa wafuasi wazuri wa dawa na mtumie kwa usahihi.”

Akizungumzia vita dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kazi ambayo asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) imekuwa ikiifanya tangu kuanzishwa kwake, Mkurugenzi huyo alisema kuwa hicho ni kipaumbele cha taifa hivyo hakina budi kufanyiwa kazi kwa juhudi.

Alisema kwa watoto na vijana wenye maambukizi, wataendelea kupata huduma za matunzo na tiba bila ubaguzi wowote ili kuhakikisha kuwa afya zao zinaendelea vizuri hivyo kuweza kufikia ndoto zao za baadaye.

“Kwa kazi zenu, AGPAHI mnagusa maisha ya Watanzania wengi. Kitendo cha kusaidia upatikanaji wa huduma za matunzo na tiba kwa wanaoishi na VVU ni cha utu. AGPAHI ni asasi ya kiutu na inajali Watanzania. Tunawashukuru kwa kuendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma hizi muhimu,” alisema.

Aidha alikumbusha kwamba kuwa na maambukizi ya VVU siyo changamoto ya kumzuia mtu anayeishi na VVU kusonga mbele katika maisha yake na kutimiza ndoto zake, “Kinachotakiwa ni kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya,” alisema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.