ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, April 20, 2019

WAKRISTO WAKUMBUSHWA KUSAMEHEANA.


Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kutumia Sikukuu ya Pasaka kutoa msamaha kwa wote waliowakosea ili kuendeleza amani ya nchi kama Yesu alivyoamua kuwasamehe waliomkosea wakati aliposulubiwa msalabani.

Akihubiri katika kanisa la Jehovah Mercy Ministry, Chanika Jijini Dar es Salaam, Nabii kiongozi wa kanisa hilo, Richard Godwin amesema njia pekee ya kuendeleza amani kwenye taifa lolote ni watu wake kusamehe wanapokoseana wao kwa wao. Amesema watu wengi wamepata magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo na hata kupoteza maisha kwa sababu ya kutosamehe.

“Usibebe mzigo mkubwa moyoni, unamshikilia mtu miaka nenda rudi hutaki kutoa msamaha kabisa. Wewe ndiye unayejiumiza na ili upate amani ya moyo wako lazima ujue kusamehe,” amesema nabii huyo na kuongeza kuwa msamaha wa kweli pia lazima uendane na utoaji wa haki.

Amesema wananchi wanaweza kuwa na amani, furaha na kusamehe ikiwa nao wanatendewa haki na mamlaka husika.

“Nikisema haki namaanisha kuna wizara inayohusika ya Sheria na Katiba ambayo mahakama ipo chini yake lakini pia, ulinzi kwa raia kupitia wizara ya ulinzi,” amesisitiza Godwin.

Amesema Pasaka ndio kipindi pekee ambacho Wakristo wanaungana pamoja kupokea wokovu unaoambatana na msamaha toka kwa mwokozi wao Yesu Kristo.

“Biblia inasema aliyabeba madhaifu yetu na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Ina maana aliteseka kwa ajili yetu maana yake tumepokea msamaha bure kabisa. Samehe ndugu yangu, uwe mtu wa haki usimuonee yeyote yule,” amesisitiza.

Mchungaji mwingine wa kanisa hilo, Paul John ‘Master Kinga’ alisema kanisa hilo limeendesha semina ya siku saba kwa waumini wake kwa ajili ya kuipokea Pasaka.

“Watu wamejua kwa nini Yesu alikufa na siku ya tatu alifufuka na wanawezaje kupokea msamaha alioutangaza?” amesema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.