ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, November 26, 2018

TRC YAJIPANGA KITEKNOLOJIA ZAIDI KABLA YA KUKAMILIKA RELI YA KISASA.


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano Isack Kamwelwe (kushoto aliyesimama) akieleza jambo kwa washiriki wa mafunzo ya uendeshaji wa mradi wa  treni ya Umeme ,SGR  alipokuwa akifungua mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam leo Novemba 26, 2018.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano Isack Kamwelwe (wa tatu kulia) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mafunzo ya uendeshaji Mradi wa Treni ya Umeme , SGR  wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi Prof. John Kondoro,  Mwakilishi wa Yapi Markez, Abdullah Kiliq kulia akishuhudia tukio hilo.


Mafunzo ya Uendeshaji  Mradi wa  SGR ni Muhimu - Waziri Kamwelwe
Na Paschal Dotto- MAELEZO
26. 11. 2018.
Waziri Kamwelwe amewataka Wahandisi wanaopata mafunzo ya uendeshaji mfumo wa reli ya kisasa (SGR) kuwa makini na mafunzo hayo ili kuwezesha uendeshwaji wa mradi huu wa kihistoria kuwa nyenzo kubwa ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam Waziri Kamwelwe amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuleta wakufunzi kutoka nchini Uturuki kuja kutoa elimu juu ya teknolojia ya kisasa ya reli ya umeme( SGR) ili kupata wataalam wa teknolojia hiyo nchini.

 “Hili tukio ni la kihistoria kwa wanareli na watanzania kwa ujumla kwa sababu mradi huu unahusisha teknolojia mpya ya usafirishaji nchini na mafunzo haya yatatoa wataalamu ambao watasaidia kuendesha mradi huu  na kusaidia sekta ya usafirishaji kwa kutumia treni ya umeme”, Waziri Kamwelwe.

Katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi Serikali imechukua mwelekeo mpya katika kujenga uchumi wa kati kwa kujenga miundombinu mbalimbali kama barabara, viwanja vya ndege, bandari pamoja na reli ya umeme itakayorahisisha usafirishaji wa mizigo.

“Kwenda kwenye uchumi wa kati kuna mambo mengi tunayotakiwa kuyafanya ndiyo maana hivi karibuni tutasaini mkataba wa ujenzi wa Stiglers Gorge kwa sababu reli tunayoijenga(SGR) inahitaji umeme wa kutosha na itakuwa na uwezo wa kutosha kwani itakuwa na mwendokasi wa kilomita 120 kwa saa kwa treni ya mizigo na kilomita 160 kwa saa kwa treni ya abiria na uwezo wa kubeba tani milioni 10,000 za mizigo”, Waziri Kamwelwe.

Aidha Waziri Kamwelwe aliwashukuru wakufunzi kuja kutoa elimu hiyo kwa awamu 11 kwani walianza na awamu ya kwanza ambayo ilichukua wanafunzi 102, awamu ya pili wanafunzi 144 huku awamu ya tatu itachukua wanafunzi 167 ambao watasoma kwa zaidi ya miezi 6 hadi mwaka 1  wakipata mafunzo.

Waziri Kamwelwe aliongeza kuwa ujenzi wa Reli ya kisasa ambao upo awamu ya kwanza yenye kilometa 1219 kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na umegawanyika katika vipande vitano yaani Dar es Salaam –Morogoro, Morogoro- Makutupola (Dodoma), Makutupola- Tabora, Tabora- Isaka (Kahama) na Isaka –Mwanza na mpaka sasa umeweza kuajiri watu 6,500.

Pia  Waziri Kamwelwe  aliwapongeza watumishi wa TRC kwa kufanya kazi kwa ufanisi na juhudi  kwani sasa shirika hilo linasimama zaidi kibiashara kwa kutoa huduma bora za kuaminika.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.