ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, November 4, 2018

MAJI HUONDOA MIGOGORO YA NDOA NA WIVU WA KIMAPENZI.




Naibu Waziri wa Nyumba Maendeleo na Makazi Angeline Mabula ambaye pia ni  Mbunge wa Jimbo la Ilemela amesema kuwa uwepo wa maji safi na salama karibu na makazi kutaondoa migogoro katika ndoa na wivu wa kimapenzi ndani ya jamii.

Waziri Mabula amesema hayo wakati alipokuwa akizindua Mradi wa Visima 7 vya maji safi na salama wilayani hapo wenye jumla ya kiasi cha fedha Tsh.28,000,000.00 uliofadhiliwa na Taasisi ya The Africa Muslims Agency, ambapo aliwaambia wananchi kuwa mfarakano na wivu wa kimapenzi utakuwa umepungua kwani awali kesi hizo zilikuwepo kutokana na mama kwenda kutafuta maji umbali mrefu na kuchelewa kurudi nyumbani.

Waziri Mabula amesema kuwa mradi huo unatarajia kutoa maji safi na salama kwa Wakazi wapatao 1750 wa Mitaa ya Chabakima, Ilalila, Bulyanhulu, Isanzu, Kadinda, Kimanilwentemi na Masemele na kuboresha usafi wa mazingira, afya ya binadamu na kuepusha magonjwa kama kipindupindu, homa za matumbo na kichocho, na kuahidi kutatua changamoto wanazokutana nazo kwani kunauhitaji mkubwa wa maji safi na salama.


Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Africa Muslims Agency Adam Osman, amesema kuwa miradi hiyo mipya itakuwa endelevu ili kuhakikisha jamii inatumia maji safi salama na kuwaomba wananchi waitumie vizuri kwa manufaa yao.

Aidha awali Mhandisi Anna Mbawala, ameeleza ujenzi wa visima virefu na na vifupi katika Wilaya ya Ilemela kupitia Taasisisi ya Kiislam ya Africa (Africa Muslims Agency) ilianza kutekeleza mradi huo kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni ujenzi wa visima vifupi vya maji saba, ambao umefanyika kuanzia Julai 2018 hadi Oktoba 2018 na kutekelezwa kwa asilimia mia katika mitaa ya Chabakima, Ilalila, Bulyanhulu, Kadinda na Kimanilwentemi.

Mbawala amebainisha kuwa mradi wa pili utaendelea katika uchimbaji wa visima vingine virefu saba katika maeneo ya Shule ya Msingi Kabusungu, Masemele, Kilabela, Shibula Sekondari na Mitaa ya Ibinza na Ibaya, ambapo ujenzi utaanza mara baada ya utafiti wa maji chini ya ardhi.

Aidha Suzan George ni mmoja kati ya akinamama waliopoteza miji yao kwa kosa la utafutaji wa maji safi na salama kwa umbali mrefu, ameshukuru mradi huo na kuwaomba wananchi kuutumia vyema kwani utasaidia kudumisha ndoa za vijana.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.