ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 16, 2018

MAJAMBAZI 7 WAUAWA NA POLISI MWANZA


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tumefanikiwa kuwaua Majambazi saba katika tukio la majibizano ya kurushiana risasi kati ya askari polisi na majambazi hao na kufanikiwa kukamata silaha mbili, silaha moja aina ya AK 47 yenye namba 56-3844714 ikiwa na magazine mbili na risasi 71 na silaha ya pili aina ya FN yenye namba 865895 ikiwa na magazine moja na risasi 5, huko katika maeneo ya milima uliopo karibu na shule ya msingi kishiri Wilayani Nyamagana.

Tukio hilo limetokea tarehe 15.11.2018 majira ya saa 22:00hrs usiku, hii ni baada kupatikana kwa taarifa za kiintelejensia kwamba katika Jiji la Mwanza wameingia majambazi wanaotaka kutenda uhalifu wakiwa na silaha za moto. Baada ya kupatikana kwa taarifa hizo Kikosi maalumu cha Makachero Mkoa Mwanza wakishirikiana na kikosi maalumu cha Makachero Mkoa wa Geita walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata jambazi mmoja aitwaye Hashim Said Abas, miaka 48, mkazi wa shamaliwa, akiwa anafuatilia eneo la kufanya uhalifu wa kutumia silaha na kupora mali katikati ya Jiji la Mwanza.

Baada ya jambazi huyo kukamatwa, askari walimhoji ndipo alikiri kwamba yeye ni miongoni mwa majambazi saba ambao wamekuwa wakifanya uhalifu wa kutumia silaha na kupora fedha na mali za watu katika mikoa ya Mwanza, Mara, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Geita na kukiri kuhusika katika matukio yakiuhalifu yafuatayo;
        i.            MWS/IR/6108/2018 Kosa mauaji ya mfanyabiashara Richard Melkiadi Slaa Wilayani Nyamagana.
      ii.             BKR/IR/516/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Mkoani Geita.
    iii.            RNZ/IR/480/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Bukombe.
  iv.            BWG/IR/643/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Chato.
    v.            Tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha katika depot ya bia Mkoani Geita.
  vi.            Tukio la Unyang’anyi wa kutumia silaha kwa mfanyabiashara  wa dhahabu katika kijiji cha Pida Wilayani Bunda.
vii.            ITL/IR/261/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Itilima.
viii.            BAR/IR/1246/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Bariadi.
   ix.            MEA/IR/552/2018 Kosa mauaji Wilayani Meatu.
     x.            ITL/IR/523/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Itilima
   xi.            ITL/1R/342/2018 Kosa unyang’anyi wa kutumia silaha Wilayani Itilima..
Pia jambazi huyo aliwaeleza askari kwamba ametumwa na wenzake ambao wapo katika mlima uliopo maeneo ya shule ya msingi kishiri ambako wameweka kambi kwa muda, kuangalia eneo la kufanya uhalifu katika Jiji la Mwanza haswaa eneo la Buzuruga ambapo kuna maduka mengi ya miamala ya fedha.

Kutokana na taarifa hizo Polisi tulijpanga vizuri kuelekea eneo hilo ambapo majambazi wenzake wameweka kambi kwa muda tukiongozwa na mtuhumiwa ndipo tulipofika karibu na eneo la tukio ghafla mtuhumiwa alitoa sauti ya neno “SHEMEJI” ishara ya kuwastua wenzake waliokuwa mafichoni ndipo walianza kufyatua risasi kuelekea kwa askari na kupelekea risasi hizo kumlenga mwenzao tuliyekua naye na kufariki dunia papo hapo. 

Askari tulichukua tahadhari ya kulala chini kisha tukaanza kujibu mashambulizi na baadae tuliwazidi nguvu majambazi hao na kufanikiwa kuwaua majambazi watatu waliokuwa wamejificha sehemu moja na kuendelea kuwafatilia wenzao watatu waliokuwa wakikimbia huku wakitufyatulia risasi lakini kwakuwa askari tulikuwa tumelizingira eneo lote vizuri tulifanikiwa kuwadhibiti na kuwaua.

Aidha katika eneo la tukio tumefanikiwa kukamata silaha mbili tajwa hapo juu zikiwa na risasi. Jambazi mmoja tu ndiye ametambuliwa jina aitwaye Hashim Said Abas, miaka 48, majambazi wengine bado hawajafahamika majina. Miili ya majambazi hao imehifadhiwa hospitali ya rufaa ya bugando kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi, pindi uchunguzi ukikamilika itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya watu  hususani vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuwa waache kwani vinaweza kuwapelekea kufungwa au kupoteza uhai hivyo wajihusishe na shughuli halali za kujipatia kipato. Sambamba na hilo tunawaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano wa kutuoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili wawezwe kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Imetolewa na;
Jonathan Shanna - ACP
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.
16 November, 2018

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.