GSENGOtV
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewaua majambazi wawili katika mapambano ya majibizano ya kurushiana risasi na majambazi hao huko katika Lodge ya Vatican iliyopo Mtaa wa Calfonia –Nyegezi kata ya Nyagezi Wilaya ya Nyamagana Jiji na Mkoa wa Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Jonathan Shanna amesema tukio hilo limetokea usiku wa Jumapili ya tarehe 07/10/2018 majira ya saa 5 na dakika 40, ikiwa ni mara baada ya kupatikana kwa taarifa toka kwa wasiri zikipasha kwamba watu wawili wameingia Jijini hapa wakiwa na silaha za moto waliopanga kufanya uhalifu na wamefikia Vatcan Lodge iliyopo mtaa Calfonia – Nyegezi.
Watu hao wanaosadikika kuwa ni Majambazi mara baada ya kufika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni walichukua chumba namba 5, na kuweka mabegi yao kisha waliondoka wakielekea eneo la katikati ya Jiji la Mwanza kwenye eneo ambalo walipanga kufanya tukio la kiuhalifu na baadaye wakarejea.
Baada ya kupatikana kwa taarifa hizo Polisi walikwenda kwa wakati katika eneo la Lodge hiyo na kuweka mtego.
Na ilipofika majira ya saa Tano na dakika Arobaini usiku, moja kwa moja Polisi walienda kwa tahadhali kwenye mlango wa chumba husika walimofikia majambazi hao na kisha wakagonga mlango mara kadhaa, wakiwataka watu hao wafungue mlango ili kuwaweka chini ya ulinzi lakini nao waligoma.
Dakika kadhaa baadae mmoja kati ya majambazi hao alifungua mlango ghafla na kufyatua risasi, lakini kutokana na umahiri wa askari waliokuwa kwenye oparesheni hiyo walifanikiwa kumpiga risasi jambazi huyo ambaye alifariki dunia papo hapo.
Wakati jambazi huyo amepigwa risasi na askari, jambazi mwingine aliyekuwa ndani ya chumba kilicholengwa, alifunga mlango na kuzima taa, kisha akavunja sehemu ya dari ya lodge ya chumba hicho na kujificha.
Polisi tulivunja mlango na kuingia ndani ya chumba hicho na kufanya upekuzi hatua kwa hatua hadi uvunguni na kuambulia patupu, lakini walipogundua kuwa kuna kiumbe kimejificha darini wasijue kinasilaha aina gani, walijihami kwa kurusha risasi za moto wakizielekeza juu mahala alipojificha.
Sekunde kadhaa baada ya kuona moto umekua mkali, jambazi hilo lilivunja paa la Lodge hiyo na kujipenyeza kwenye bati nje na kisha kuruka ukuta na kuanza kukimbia.
Polisi walifyatua risasi kadhaa hewani wakimuamuru mtuhumiwa kusimama na kujisalimisha naye alikaidi amri hiyo, ndipo walipoamua kurusha risasi iliyomlenga, naye alikimbia umbali wa makadirio ya mita 100 toka ilipo lodge hiyo, na baadaye kuanguka na kufariki dunia papo hapo.
Aidha katika tukio hilo, Polisi imefanikiwa kukamata silaha moja iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za silaha aina ya short gun (Home made gun). Pia upekuzi ulifanyika katika chumba walichofikia majambazi hao na kupata risasi tano za silaha aina ya short gun ambazo hazijatumika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, linatoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuendelee kutoa taarifa, pindi wanapotilia shaka wageni wanaoingia maeneo mbalimbali.
Kamanda Shanna ametoa onyo kwa wale wote waliogeuza uhalifu kuwa ajira zao na kwamba Mwanza wataingia lakini hawatatoka. "Labda wakafanye shughuli zao haramu za ujambazi Kuzimu lakini siyo Mwanza, Hawa wameingia lakini hawajatoka salama" Alimaliza kamanda Mshana.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.