Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio za Rotary Dar, Catherinerose Barretto (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika leo (Oktoba 02, 2018) jijini Dar es Salaam kutangaza rasmi maandalizi ya mbio na matembezi ya hisani ya Rotary Dar yanayotarajia kufanyika Oktoba 14 mwaka huu (Siku ya Mwalimu Nyerere). Pamoja na mambo mengine mwaka huu Kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi imeongeza hatua nyingine zaidi kwa ajili ya kutangaza michezo Tanzania kwa kutoa ufadhili kwa Mtanzania mwanaume na mwanamke atakayefanya vizuri katika mbio za kilomita 42.2, ambao wote watapelekwa kushiriki mbio za Beirut nchini Lebanon.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC Tanzania, Rashid Chenja (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo (Oktoba 02, 2018) jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kutangaza rasmi maandalizi ya mbio za Rotary Dar zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu (Siku ya Mwalimu Nyerere). Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi wa Mbio za Rotary Dar, Bi. Sharmila Bhatt na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha riadha Tanzania (CRT) Ombeni Zavara.
Msanii wa kike anayetamba zaidi nchini, Vanessa Mdee al-maarufu Vee-Money ambaye pia ni Balozi wa Mbio za Rotary Dar kwa mwaka huu akizungumza leo (Oktoba 02, 2018) jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kutangaza rasmi maandalizi ya mbio za Rotary Dar zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu (Siku ya Mwalimu Nyerere). Vanessa atashiriki mbio za Rotary Dar kwa mwaka huu lakini pia atatumia ushawishi alionao kuwahamasisha watu wengi zaidi kushiriki. Pamoja nae ni Mwenyekiti wa Bodi wa Mbio za Rotary Dar, Bi. Sharmila Bhatt (kulia) na Mkurugenzi Uendeshaji wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto).
Mkurugenzi Uendeshaji wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto) akionyesha kipeperushi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo (Oktoba 02, 2018) jijini Dar es Salaam kuelezea baadhi ya huduma maalumu zinazotolewa na hospitalini hapo wakati wa hafla ya kutangaza rasmi maandalizi ya mbio za Rotary Dar zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu (Siku ya Mwalimu Nyerere). Pamoja nae ni Msanii Vanessa Mdee al-maarufu Vee-Money (katikati) ambaye pia ni Balozi wa wa Mbio za Rotary Dar kwa mwaka huu na Mwenyekiti wa Bodi wa Mbio za Rotary Dar, Bi. Sharmila Bhatt (kulia).
Dar es Salaam. Mwaka huu unaweka alama ya maadhimisho ya miaka 10 ya Mbio za Rotary Dar, tukio la hisani ambalo limekuwa likiweka rekodi kubwa katika usajili kila mwaka.
Kupitia mbio hizo,miradi mbalimbali ya huduma za kijamii imekuwa ikitekelezwa kwa miaka tisa mfululizo iliyopita kupitia fedha ambazo huwa zinachangwa ikiwemo upandaji miti zaidi ya 26,000,utoaji wa huduma ya maji safi ya kunywa shuleni,
Ujenzi wa wodi ya saratani ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kituo cha maendeleo ya ujasiriamali Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka huu, matembezi ya hisani na mbio za Rotary Dar zinalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa kliniki maalum katika Hospitali ya CCRBT itakayowezesha utoaji huduma na kupunguza gharama zinazotolewa kwa watu wenye ulemavu.
Mbio za Rotary Dar ni juhudi za pamoja baina ya klabu nane za Rotary jijini Dar es Salaam ambazo zimekuwa zikiungwa mkono kwa ufadhili mkubwa wa Benki M na Pepsi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi wa Mbio za Rotary Dar, Bi. Sharmila Bhatt amesema, "Tunaamini ushirikiano wa kimkakati tuliokuwa nao na Benki M ulikuwa na mafanikio makubwa jambo lilopelekea muelekeo mzuri na kutoa motisha kwa wafadhili wengine katika ambao wanatuunga mkono mwaka huu," alieleza na kuongeza kuwa, "mwaka huu Pepsi nao wameongeza hatua nyingine zaidi kwa ajili ya kutangaza michezo Tanzania kwa kutoa ufadhili wa jumla kwa Mtanzania mwanaume na mwanamke atakayefanya vizuri katika mbio za kilomita 42.2, ambapo watapelekwa kushiriki mbio za Beirut Marathon nchini Lebanon.
Haya ni mafanikio makubwa kwa Mbio za Rotary Dar, kukubalika na kuweza kutoa Watanzania watakaoshiriki riadha kwa kupewa ufadhili kwa ajili ya mbio za Kimataifa".
Pia alitaja wadau wengine muhimu katika ufadhili huo wa Mbio za Rotary Dar kuwa ni Ashton Media, Toyota, ALAF, Zoom Tanzania, Resolution Insurance,Clouds Media Group, Azam Media, Plasco Limited, Insignia, Night Support, Ashers na Soft Tech.
Bi. Bhatt alitumia pia fursa hiyo kumtambulisha Balozi wa Mbio za Rotary Dar 2018, msanii wa kike anayevuma zaidi nchini Bi. Vanessa Mdee al-maarufu Vee-Money ambaye atashiriki katika matembezi na mbio hizo ikiwemo kutoa hamasa na motisha kwa washiriki wa tukio hilo ili wajitokeze kwa wingi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bi.Vanessa ameeleza kuupokea ubalozi huo kwa moyo mweupe huku akiahidi kuunga mkono tukio hilo.
"Ninafarijika sana kupewa fursa kubwa kama hii na nimeamini kuwa ninaweza kufanya jambo kuhusiana na tukio hili kwa jamii. Ninaahidi kututumia ushawishi wangu ili kuvutia washiriki wengi zaidi. Nikitambua kuwa kila mshiriki atakayeshiriki katika tukio hili, uchangiaji wake utawezesha kusaidia wengine,"amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mbio za Rotary Dar 2018, Rotarian Catherinerose Barretto aliwahakikishia Watanzania kuwa, kila kitu kinaenda vizuri, kama kilivyopangwa. Aliongeza kuwa, Oktoba 14, 2018 itakuwa siku ya kumbukumbu kwa michezo na siku ya tukio la kifamilia katika historia ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Bi. Barretto miaka 10 ya Mbio za Rotary Dar zinatarajiwa kuwavutia zaidi ya washiriki 16,000.
Amesema, tukio hilo litahusisha matembezi ya familia kilomita tano, matembezi ya kilomita tisa, mbio za kilomita 21.1, mbio za kilomita 42.2, baiskeli na shughuli nyingine nyingi za kufurahisha.
"Tunatarajia kuwa na washiriki kutoka Kenya,Uganda, Rwanda, Malawi, Afrika Kusini na Ethiopia, "amesema.
Bi. Barretto alikumbushia kuwa, kauli mbiu ya tukio hilo itaendelea kuwa, "Ponya Maisha, Badilisha Jamii" ikiwa ni mwaka wa tatu wakichangisha fedha kwa ajili ya kuisaidia Hospitali ya CCBRT iweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa CCBRT, Bi. Brenda Msangi kujengwa kwa kiliniki ya kisasa hospitalini hapo kutasaidia kuimarisha juhudi za utoaji huduma ikiwa matarajio yao ni kuhudumia Watanzania wengi zaidi miaka ijayo.
"Mbio za Rotary Dar kila wakati zimekuwa zikifikiria namna ya kuisaidia hospitali yetu katika uendeshaji wa shughuli zetu. Na matokeo yake ni kuwa jamii kubwa ya Watanzania inanufaika kupitia moyo wao wa kujitoa,"amesema.
KUHUSU ROTARY
Rotary ni taasisi ya huduma ambayo ilianzishwa mwaka 1905, Chicago, Illinois ambayo ina wanachama zaidi ya milioni 1.2 duniani nao hujitoa kwa moyo wa upendo kusaidia.
Ikiwa na vilabu 35,000 Duniani kote, watu kutoka mabara yote na tamaduni uungana pamoja kubadilishana mawazo,kuanzisha urafiki,kushirikishana fursa za kitaaluma ili kuleta mabadiliko chanya duniani.
Kila siku wanachama wetu hujitoa kwa moyo kwa ajili ya kusaidia huduma mbalimbali zinazoleta mabadiliko kwa wengi.
Tunajikita katika kuhamasisha amani, kutoa huduma ya maji safi,kupambana na magonjwa,kusaidia mama na mtoto,elimu ikiwemo miradi ya kiuchumi katika jamii.
Hapa Tanzania Rotary ilianza mwaka 1945 ambapo ina vilabu 38 na wanachama 600.
Katika Jiji la Dar Es salaam kuna vilabu nane ikiwemo The Rotary Club of Dar es Salaam, Dar es Salaam Mikocheni, Dar es Salaam Mlimani, Dar es Salaam North, Dar es Salaam Mzizima,Dar es Salaam Pugu na Dar es Salaam Oysterbay.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.