Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa katika msimu wa Novemba 2018 hadi Aprili 2019 katika kanda za magharibi, kati na nyanda za juu kusini.
Maeneo yatakayoathirika na mvua hizo za juu ya wastani hadi wastani ni Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, Kusini mwa Morogoro, Lindi na Mtwara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi amesema utabiri huo ni kwa mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
"Katika kipindi cha mvua za msimu hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi,” amesema.
"Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi kama vile mahindi, maharage na mtama yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama.”
Kutokana na mvua hizo, Kijazi amewatahadharisha pia wachimbaji wa madini hasa wadogo kuwa makini na ongezeko la maji linaloweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi au maji kujaa kwenye mashimo.
Pia, amezishauri mamlaka za miji na majiji kuchukua tafadhali kwa kuhakikisha mifumo ya kupitisha maji inafanya kazi ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko yanayogharimu maisha ya watu na uharibifu wa miundombinu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.