ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 5, 2018

OSHA YATOA SEMINA KWA WANAHABARI MWANZA.

Kaimu  mtendaji mkuu wa Taasisi ya OSHA Khadija Mwenda  akitoa darasa kwa waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (wanaonekana katika picha za chini).
WAKALA wa Usalama na Afya mahali pa kazi(OSHA) imetoa semina ya siku  mmoja kwa waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza kaka sehemu ya mkakati wake wa kufikia wadau.

Akizungumza leo, Kaimu  mtendaji mkuu wa Taasisi ya OSHA Khadija Mwenda  alisema kupitia wanahabari ambao ni nguzo muhimu katika jamii ,itawasaidia wanajamii kuweza kujua  jinsi gani ya kufanya kazi wakiwa makazini  kwao. 

Alisema kumekuwa maswali mengi kuhusiana na OSHA.

Alisema taasisi yao ina  mikakati yakuendelea kuongeza uelewa kwa wadau na wanahabari ambao ni wadau wakubwa. 

Aliahidi kampuni yao imeondoa gharama za usajili na kwa sasa usajili ni bure. Khadija alisema wataendesha oparesheni maalumu ya kikanda kuhakikisha maeneo ya kazi yamesajiliwa.
Je sheria ya Usalama na Afya sehemu za Kazi ya mwaka 2003 inagusa sehemu gani?
Sheria hii inagusa viwanda vyote na sehemu zote za kazi ambazo hazijapatiwa msamaha na Waziri kama sheria inavyosema.

Je sheria imeweka wajibu wa mfanyakazi?
Ndio, Zifuatazo ni baadhi ya wajibu wa mfanyakazi uliowekwa na sheria: 
• Wafanyakazi ni lazima wachukue tahadhari za makusudi dhidi ya usalama na afya   zao na mtu mwingine ambaye anaweza kuathirika na vitendo vyao au kutokuepo kwako kazini.
• Vile vile wafanyakazi wana wajibu wa kushirikiana na Waajiri ili kuwezesha mahitaji   yaliyowekwa na Waajiri kufikiwa au kuzingatiwa kwa usahihi. 
• Wafanyakazi pia wana wajibu wa kutekeleza amri yeyote kisheria walizopewa na zinazo heshimu kanuni na taratibu za afya na usalama zilizowekwa na Waajiri au mtu mwenye mamlaka kwa madhumuni ya kulinda afya na kuhakikisha usalama.
• Kutoa taarifa kwa mwajiri au mwakilishi wa usalama na afya sehemu za kazi juu ya kuwepo kwa hali isiyokuwa salama au yenye madhara kiafya inayojitokeza sehemu za kazi.
• Kutoa taarifa kwa mwajiri au mwakilishi wa usalama na afya sehemu za kazi juu ya hali yoyote au ajali ambayo inaweza kusababisha madhara kwa afya zao mapema iwezekanavyo ( sio zaidi ya mwisho wa zamu labda kama hali imepelekea hivyo)
Pichani:- Kaimu Meneja  OSHS Kanda ya Ziwa Mjawa Mohamed Shenduli akitoa darasa kwa waandishi wa habari jijini Mwanza.
Mwajiri ana wajibu gani chini ya sheria hii?
Wajibu wa mwajiri chini ya sheria ya Usalama na Afya sehemu za Kazi ni kama ifuatavyo:
• Kusajili eneo lake la kazi na Wakala wa Usalama na Afya sehemu za kazi
• Kupima afya za wafanyakazi mara kwa mara kwa kuzingatia sheria.
• Kuchagua mwakilishi wa usalama na afya sehemu za kazi katika sehemu yenye wafanyakazi wanne na zaidi. 
• Mwajiri ni lazima ahakikishe mahali pa kazi ni salama kiafya na hatakiwi kuruhusu mfanyakazi kufanya kazi yenye madhara au hatarishi. 
• Ni lazima wawape wafanyakazi taarifa juu ya hatari iliyopo katika eneo la kazi
• Ni lazima wahakikishe hatari imedhibitiwa hadi hatua ya chini kabisa kabla ya kutoa vifaa vya kujikinga.
• Ni lazima watoe nguo za kujikinga pale inapolazimu. 
• Ni lazima watoe mafunzo kwa wafanyakazi wanaotumia mashine na vifaa hatarishi kuhakikisha wanafahamu hatua za kiusalama. 
• Ni lazima wawazuie wafanyakazi kutumia au kufanya kazi na vitu au mashine hatarishi mpaka kanuni zote za usalama zifuatwe.
• Ni lazima ahakikishe kwamba mashine hatarishi zinafanya kazi vizuri na ziko salama kuzitumia.
• Ni lazima wahakikishe kuwa mashine hatarishi zina tahadhari au notisi kuonyesha kua ni hatari.
• Ni lazima wahahkishe kuwa mtu anyejua kazi anasimamia utendaji kazi kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.
• Ni lazima waache sehemu za kazi wazi ili kuruhusu wafanyakazi kutoka inapotokea hatari.
Je kuna adhabu yoyote pale ambapo mfanyakazi au mwajiri anakikiuka sheria?
Inapotokea ajali iliyosababishwa na mwajiri na ikamuumiza au hata kumuua mfanyakazi basi mwajiri atawajibika kulipa fidia isiyopungua milioni kumi (10) au kutumikia kifungo cha kipindi kisichozidi miaka miwili(2) au kufungwa na kulipa fidia kwa pamoja. Mahakama pia inaweza kuongeza juu ya fidia au badala ya fidia kutoa amri kuondolewa kwa kilichosababisha tatizo. 
Kama mfanyakazi atavunja au ataenda kinyume na sheria ilivyosema basi atawajibika kulipa faini au kufungwa au kupata vyote ( kifungo na faini) kutegemea na kosa lenyewe. 
Je mwajiri anaweza kumuadhibu mfanyakazi kwa kulalamikia hali ya usalama?
Hapana, sheria inamkataza mwajiri kumfuta mtu kazi, kupunguza mshahara na marupurupu yake, kubadilisha vigezo na masharti ya mkataba wa kazi kwa sababu zifuatazo:
•    Kutoa ushahidi mahakamani kuhusu hali zao za kazi.
•    Kujibu maombi au maswali ya mkaguzi
•    Kukataa kufanya chochote ambacho ni kinyume na sheria
•    Kutoa taarifa kuhusu hali zao za kazi
•    Kutii vikwazo vya kisheria, mahitaji, maombi au maelekezo yatolewayo na wakaguzi
•    Kupata magonjwa yatokanayo na kazi na hata yale mengine yasiyotokana na kazi 
Je mwajiri anatakiwa kutoa taarifa za ajali zitokeazo sehemu za kazi?
Mwajiri ana wajibu wa kutoa taarifa juu ya tukio au ajali yoyote iliyotokea eneo la kazi na kupelekea kifo, maumivu au majeraha ya mwili, kupoteza fahamu, magonjwa yatokanayo na kazi au yamempa ulemavu wa moja kwa moja mfanyakazi, ndani ya saa 24 kutoka tukio au ajali kutokea. Ndani ya siku saba kutoka tukio au ajali kutolewa taarifa mwajiri anatakiwa kutuma taarifa kamili inayoelezea tukio au ajali hiyo. 

Ni namna gani vipengele vya sheria hii vinasimamiwa na kuhakikisha vinatekelezwa?
Wakala wa Usalama na Afya sehemu za kazi (OSHA) iliyoanzishwa chini ya sheria ya wakala wenye kutoa maamuzi Na. 30 ya mwaka 1997 ndio wasimamizi wa sheria Na. 5 ya usalama na afya sehemu za kazi ya mwaka 2003.
Malengo ya msingi ya Wakala wa usalama na afya sehemu za kazi (OSHA) ni kuhakikisha kuanzishwa na kuendelea kuwepo na mazingira salama ya kazi ambayo ni huru dhidi ya madhara yatokanayo na kazi amabyo yanweza kupelekea kuumia au magonjwa kwa wafanyakazi katika eneo la kazi. Wakala wameajiri wakaguzi wa kazi ambao moja ya wajibu wao ni ukaguzi wa afya na usalama sehemu za kazi. Baada ya kuandaa ripoti, hupelekwa kwa mkaguzi mkuu kwa ajili ya kuchukua hatua ambazo zinaweza kua:
•    Kumshauri mwajiri ipasavyo.
•    Kutoa notisi ya kuboresha hali.
•    Kutoa notisi ya kuzuia.
•    Kupeleka suala mahakamani. 

Pichani:- Kaimu Meneja  OSHS Kanda ya Ziwa Mjawa Mohamed Shenduli akitoa darasa kwa waandishi wa habari jijini Mwanza.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.