ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, September 1, 2018

DKT. BASHIRU ASEMA MIKATABA UWEKEZAJI CCM YA-KIFISADI.





Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema mikataba ya uwekezaji katika chama hicho na jumuiya zake, inatarajiwa kupitiwa upya kwa kuwa baadhi ni ya kifisadi na kitapeli.

Dk,. Bashiru alisema hayo jana jijini hapa wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), huku akibainisha kuwa umoja huo ndio unaoongoza kuwa na mikataba mingi mibovu.

Alisema lengo la kuipitia upya mikataba hiyo ni kujadiliana kwa misingi ya usawa na hakutakuwa na mkataba ambao chama au jumuiya inapoteza umiliki wake.

Aidha, alisema limeshaundwa baraza la wadhamini wa chama ambalo kwa mujibu wa Katiba ya CCM, lina mamlaka ya kusimamia mali zote za chama na jumuiya zake.

“Yale yote mabaraza ya Jumuiya yaliyokuwapo yalikuwa uchochoro wa wizi na uporaji wa mali za jumuiya na yamefutwa kikatiba,”alisema.

Dk. Bashiru alisema wakati wa uhakiki wa mali za chama kuna mambo yalionyesha kuwa jumuiya hiyo imeanza kupoteza misingi ya nidhamu.

“Mali zenu nyingi zimekuwa hazitumiki vizuri. Ni jumuiya ambayo ina mikataba mibovu na hasa mkataba wa mradi wenu mkubwa pale Dar es Salaam, ni mkataba wa wizi, wa kitapeli,” alisema.

Alibainisha kuwa, chama kimedhamiria kuchukua taratibu za kisheria kurejea mikataba hadi ifike mahali ambapo mwekezaji na umoja huo wanakuwa sawa.

“Hatutaki mikataba ambayo chama au jumuiya inapoteza umiliki wake kama yaliyopo pale kwenye miradi yenu jijini Dar es Salaam. Mikataba ile pamoja na mambo mengine mmepoteza haki ya kumiliki wa ardhi yenu,” alisema.

Alifafanua kuwa, katika moja ya mikataba mwekezaji ametumia hati kukopa na kwamba mkataba huo UVCCM inapata asilimia 25 huku mwekezaji asilimia 75.

“Sasa kwa nini msifanye kama Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wao wameenda kukopa halafu wanajenga halafu watalipa kutokana na uwekezaji waliopata,” alisema huku akisisitiza kuwa: “Mikataba ya aina hiyo imefika mwisho na haitatokea mikataba tena kama hiyo.”

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru aliwataka vijana kuendesha mijadala inayohusu demokrasia katika mitandao ya kijamii ili kuimarisha uhuru wa kujitawala, amani na utulivu.

Aidha, aliwataka viongozi wa UVCCM kuhakikisha wanafanyia kazi suala la ukomo wa madaraka ndani ya jumuiya hiyo kwa kuondoa viongozi au kutochagua viongozi ambao umri wao kikanuni hauruhusiwi.

Akimkaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Umoja huo, Kheri James, aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuchagua watu wenye sifa na uzalendo ndani ya chama na si kuchagua watu ambao ni vibaraka.

Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Raymond Mwangwala, alisema tangu Katibu Mkuu wa chama aanze kazi sasa ni siku 100 na kwamba amefanya mapinduzi na mabadiliko makubwa ndani ya chama.

Aliwataka vijana hao kuhakikisha wanatetea maslahi ya chama na taifa kwa ujumla badala ya kujikita kwenye mitandao ya kijamii na kwamba wawe mstari wa mbele kumtetea Rais John Magufuli kutokana na utendaji anaofanya.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.