Mji mkuu wa Uganda Kampala, leo umeshuhudia malalamiko na maandamano baada ya polisi kuwatia mbaroni wabunge wawili wa upinzani wakiwa katika harakati za kuelekea nje ya nchi kwa matibabu.
Wabunge wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na Francis Zaake walitiwa mbaroni jana usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe wakiwa katika pirikapirika za kutaka kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Wakili wa mbunge Bobi Wine amesema kuwa, mteja wake alizuiwa kuingia katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Entebbe na kuchukuliwa na polisi ambao wanadaiwa kumpeleka katika hospital ya serikali.
Maandamano ya leo ya wafuasi wa wabunge hao yameshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Kampala ambapo waandamanaji wenye hasira waliweka vizuizi barabarani na kuchoma moto matairi.
Vikosi vya usalama vilikuwa na kazi ya ziada kuzima maandamano hayo na kusafisha barabara zilizokuwa zimejaa vizuizi.
Mbunge Bobi Wine ambaye amejizolea umashuhuri mkubwa hivi karibuni nchini Uganda anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni katika kampeni za uchaguzi mdogo huko Arua. Bobi Wine aliachiliwa kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa siku ya Jumatatu, akiwa katika hali mbaya kiafya.
Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, wabunge hao akiwemo Bobi Wine waliteswa vibaya wakati walipokuwa kizuizini, ingawa serikali ya Kampala kupitia msemaji wake Ofwono Opondo ilisisitiza tena wiki iliyopita kwamba, taarifa za kuteswa wabunge hao ni za uwongo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.