ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, August 5, 2018

WALE WOTE WALIOFANYA UFISADI WAJIANDAE KUITWA



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema wale wote ambao wamefanya ufisadi wajiandae kuitwa na ofisi yake akiwamo aliyelipwa mabilioni ya kutengeneza sare za Jeshi la Polisi.

Awali Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilimhoji kada wa Chama Cha Mapinduzi na Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa tuhuma za kutosambaza sare za Jeshi la Polisi licha ya kulipwa Sh. bilioni 40 na serikali.

Kuhojiwa kwa mbunge huyo ni baada ya Rais John Magufuli kuibua sakata hilo mwaka 2016 kwa kudai kuna fedha zimelipwa kwa ajili ya kununua sare za Jeshi la Polisi tangu mwaka 2015, lakini hazikununuliwa.

Akihojiwa na Nipashe jana kwa njia ya simu, Lugola alisema kuwa maagizo aliyopatiwa na Rais Magufuli ambayo yanagusia baadhi ya Watanzania ambao wana tuhuma za ufisadi ikiwamo la sare la Jeshi la Polisi pamoja na yale ambayo hajayasema atayashughulikia.

Lugola alisema hakuna ambaye hataitwa, hivyo asidhani kwamba kazi imeisha ajiandae wakati wowote ataitwa na hatua zitachukuliwa.

"Mimi nawajibika kufuatilia na kuwabaini mafisadi wote kokote walipo hata kama wamejificha uvunguni, wakimbilie chooni ama vichakani lazima nitawasaka na kuwakamata mmoja baada ya mwingine ikithibitika tunamfikisha kwenye mahakama ya mafisadi,” alisema.

Aliongezea kuwa: “Hakuna ambaye atapona sio kwa sababu tumeshughulika na Lugumi basi wakadhani Lugumi ndio mwisho hapana... wote waliofanya ufisadi wataitwa hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa kila jiwe litageuzwa,” alisema Lugola.

Mwaka juzi, Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na maofisa wa Jeshi la Polisi aliowapandisha vyeo vya Naibu Kamishna wa Polisi na Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Ikulu jijini Dar es Salaam aliibua sakata hilo.

Rais Magufuli alisema ana taarifa za rushwa ndani ya Jeshi la Polisi inayokadiriwa kuwa kati ya Sh. bilioni 40 na Sh. bilioni 60 ambazo zilipaswa kununulia sare kwa ajili ya askari polisi tangu mwaka 2015, lakini hazikununuliwa.

Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwa kampuni ambayo ilipendwa zabuni ya Daissy General Traders ilikuwa kampuni hewa.

Mbali ya kwamba ni kampuni ya mfukoni, uchunguzi huo pia ulibainika taarifa za awali zilionyesha inajihusisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, aliiambia Nipashe Januari 13, mwaka jana kuwa kampuni hiyo ni hewa kwa sababu walishindwa kubaini zilipo ofisi zake.

Rwegasira alisema awali waliambiwa Daissy General Traders ina ofisi katika makutano ya mitaa ya Uhuru na Swahili, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

WATU WALIPEANAKutokana na maelezo hayo katika anuani ya kampuni hiyo, Rwegasira alisema walifuatilia, ili kujiridhisha kama ziko sehemu hiyo, alisema lakini walipofika hawakukuta ofisi hizo.

Jambo hilo liliwafanya wakabidhi kazi hiyo kwa Takukuru, ili ichunguze zaidi.

Katibu mkuu huyo mstaafu alisema kuna uwezekano kwamba kuna watu walipeana zabuni hiyo na kampuni ambayo ni ya mfukoni isiyokuwa hata na ofisi na ndiyo maana walishindwa kuipata ilipo.

Inadaiwa kuwa kampuni hiyo iliingia mikataba na Polisi kati ya mwaka 2013-2016, lakini katika kipindi chote hicho ilishindwa kusambaza hata sare moja.

Mwaka jana Takukuru ililieliza Nipashe kuwa tayari wamemhoji kigogo huyo na kwamba uchunguzi unakaribia kukamilika.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.