ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, August 5, 2018

6 KIZIMBANI KWA KUJINUFAISHA NA ZABUNI.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewapandisha kizimbani watu sita wakiwemo watatu waliokuwa watumishi wa mgodi wa serikali wa Stamigold wilayani Biharamulo.

Vigogo hao wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya Wilaya ya Biharamulo kwa kile kilichoelezwa kuwa walijinufaisha na zabuni za mgodi huo.

Wengine watatu ni wa makampuni mawili yaliyopewa zabuni za kutoa huduma kwenye mgodi huo ambao wanatuhumiwa kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa mgodi wa Stamigold.

Ofisa uhusiano wa Takukuru, Mussa Misalaba katika taarifa yake amesema kuwa washitakiwa walipandishwa kizimbani Agosti 3, 2018 mbele ya Kaimu hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Biharamuro ambaye pia ni Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Biharamuro, Esdward Samala.

Hatua ya kuwapandisha kizimbani vigogo hao imekuja kufuatia agizo la Waziri wa Madini Angela Kairuki alilotoa Oktoba 27, mwaka jana, akiitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwasilisha taarifa zote za gharama za uendeshaji wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa STAMIGOLD – Biharamulo ili kujiridhisha pamoja na kuchukua hatua za kisheria iwapo kama kuna taratibu za manunuzi zimekiukwa.

Kairuki alitoa agizo hilo alipofanya ziara katika mgodi huo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera lengo likiwa ni kufahamu shughuli za migodi ya serikali, binafsi na wachimbaji wadogo.

Waziri Kairuki alibaini gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za mgodi huo pamoja na madeni hali inayopelekea shirika hilo kujiendesha kwa hasara badala ya kujiendesha kwa faida.

Mwendesha mashitaka wa Takukuru Dismas Muganyizi amewataja watumishi hao kuwa ni Meneja wa fedha wa mgodi,Clara Mwaikambo, Meneja Uchenjuaji wa dhahabu, Christopher Mwinuka na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi , Sadick Kasuhya.

Wengine waliopandishwa kizimbani ni Wakurugenzi wa kampuni ya Super core Drilling, Reginald Haule na mwajiriwa wa Supercore Drilling, Fortunatus Luhemeja, na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Waja General, Chacha Wambura.

Upande wa mashitaka umeiambia mahakama kuwa makampuni ya utoaji huduma yalipata zabuni baada ya kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa Stamigold kati ya mwaka 2015 na 2016.

Katika kipindi hicho Kampuni ya Super Core ilipewa zabuni ya kutoa huduma ya uchorongaji miamba na kampuni ya Waja General ilipewa zabuni ya kuuza kemikali za uchenjuaji wa dhahabu.

Kwa kuwa Hakimu Samala hakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo wala kutoa dhamana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kuhusiana na kesi hiyo na kesi imeahirishwa hadi Agosti 6, 2018 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Francis Jesse, Mashauri Miyasi

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.