ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 27, 2018

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA CHARLES KABEHO, AGOMA KUFUNGUA MRADI WA KITUO CHA UPASHANAJI HABARI ZA MAFUNZO YA KILIMO NA MIFUGO KWIMBA MKOANI MWANZA.


NA ZEPHANIA MANDIA/GSENGOtV

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Charles kabeho, amegoma kufungua Mradi wa Kituo cha Upashanaji habari za Mafunzo ya Kilimo na Mifugo kilichojengwa kijiji cha Mhande wilaya ya Kwimba kwa Sh milioni 69, akidai maelezo ya kina juu ya thamani halisi ya samani zilizonunuliwa na kuwekwa hapo. 


Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. John Mongella ameongoza shamra shamra za mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Shule ya Msingi Izizimba A wilayani Kwimba jana Agosti 26, 2018 ukitokea mkoani Shinyanga.
MWENGE wa Uhuru umeingia Mwanza huku Kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Charles Kabeho akionya mwenge huo hautafungua miradi iliyojengwa chini ya kiwango na isiyokidhi thamani halisi ya fedha iliyowekezwa.
Ametoa onyo hilo baada ya mapokezi ya mwenge uliowasili kutoka mkoani Shinyanga.
Kabeho amesema uzoefu wa baadhi ya miradi aliyofungua huko nyuma umeonesha haikidhi viwango na mingine haioneshi mtiririko mzuri wa thamani ya vifaa vilivyotumika kwa ujenzi.
Baada ya kuanza mbio na kudhihirisha kauli yake, alikataa kuzindua kituo cha upashanaji habari za Kilimo na Mifugo kilichojengwa kijiji cha Mhande wilaya ya Kwimba kwa Sh milioni 69, akidai maelezo ya kina juu ya thamani halisi ya samani zilizonunuliwa na kuwekwa hapo.
Mbele ya jengo lililoleta utata.
Jiwe la msingi la Jengo lililogomewa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru.
"Mwenge hautafungua kituo hiki na ninaiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ifanye uchunguzi juu ya gharama zilizotumika kwa ununuzi wa samani," amesema.
"Mahesabu yamegoma".....
Taarifa iliyosomwa mapema juu ya ujenzi wa kituo hicho ilionesha samani zake ziligharimu zaidi ya Sh milioni 15 ingawa mwonekano wake ulimtia shaka kiongozi huyo na akaamuru uchunguzi wa kina ufanyike kubaini ubadhirifu.
Miradi 56 yenye thamani ya Sh bilioni 13 inatarajiwa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru ulioanza mbio zake mkoani Mwanza hapo jana.
Mapema akisoma taarifa ya mkoa kwa kiongozi wa mbio hizo mpaka wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga ulioko eneo la Kazizimba A kata ya Mande wilayani Kwimba jana, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema miradi 17 ya Sh bilioni 5.8 itawekewa mawe ya msingi.
Alisema miradi 17 ya thamani ya Sh bilioni 2.8 itazinduliwa, 12 ya Sh bilioni 2.3 itafunguliwa na mingine 10 ya Sh bilioni 2.6 kukaguliwa.
"Miradi hii yote imegharamiwa na serikali kuu kwa Sh bilioni 5.8, halmashauri kwa Sh bilioni 1.3, nguvu za wananchi Sh bilioni 1.9 na wahisani mbalimbali Sh bilioni tano," alisema.
Alisema serikali ikishirikiana na wananchi inawekeza ujenzi wa miundombinu na akataja mfano wa ukarabati wa majengo yaliyochakaa ya shule nne kongwe za sekondari Mwanza.
Alitaja shule hizo ni Bwiru Wasichana, Bwiru Wavulana, Nganza na Sengerema zilizotumia zaidi ya Sh bilioni 3.7 kuzifanyia ukarabati.
Sambamba na ukarabati huo, Mongela alisema Sh milioni 983 zimetumika kwa ujenzi wa hosteli za shule zenye kidato cha tano na sita za Nyehunge, Bukongo, Mwamashimba na Pius Msekwa wakati uwekezaji mwingine ni kwenye ujenzi wa matundu 276 ya shule za msingi 62. Mongella alisema ukarabati na uimarishaji wa miundombinu umeongeza idadi ya wanafunzi waliodahiliwa elimu ya msingi na sekondari.
Alitoa mfano wa mwaka 2015 ambapo udahili ulikuwa wanafunzi 107,221 hadi 127,746 mwaka huu na sekondari kutoka wanafunzi 37,017 mwaka 2015 hadi 49,046 mwaka huu.
Kwenye eneo la afya, Mongela alitoa taarifa mpya za maambukizi ya Ukimwi takwimu zikionesha yamepungua kutoka asilimia 15.1 mwaka 2016 hadi asilimia 8.1 mwaka huu.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.