Akiongea na wajumbe wa kikao hicho, Mhe. Mhandisi Gabriel alianza kwa kuwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kutoa taarifa sahihi, lakini pia kuwashukuru waratibu wa mpango huo kuanzia ngazi ya Sekretarieti ya Mkoa hadi ngazi za Halmashauri na kusema kuwa, ni imani yake kikao hicho kitaweka mikakati thabiti ili kupata matokeo chanya. Ni baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo, ndani ya ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 12.07.2018.
Mkuu wa Mkoa aliendelea kwa kusema “nimeona mabadiliko makubwa ,nimefurahishwa na mashamba ya pamba ambayo yanamilikiwa na walengwa wa mpango. Nawashukuru sana viongozi kwa usimamizi mzuri, hivyo ni vyema viongozi kuendelea kuzitembelea kaya hizi na kila mmoja kwa nafasi yake, kwenye eneo lake, ahakikishe TASAF awamu hii inakuwa yenye manufaa kwenye eneo husika lakini walengwa wanaondokana na umasikini kupitia ufuatiliaji wa karibu ili nia ya Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kufanikiwa”.
Akisoma taarifa ya utekelezaji, Mratibu wa TASAF ngazi ya Mkoa Bw. Elikana J. Harun alieleza kuwa, Mkoa wa Geita umehawilisha jumla ya Shilingi Bilioni Ishirini na Tatu, Mia Sita Themanini Milioni, Sitini na Nane Elfu na Hamsini na Nane (Tshs.23,680,068,058) sawa na asilimia 98.32 ya fedha zilizopokelewa ili kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini – TASAF awamu ya Tatu kuanzia Julai 2015/2016 hadi Juni, 2017/2018, kazi iliyofanyika kwa vipindi 18 katika Mitaa 27 na Vijiji 321 vilivyoingizwa kwenye mpango huo kwenye halmashauri sita za Mkoa wa Geita, Bw. Harun aliyataja mafanikio mbalimbali waliyoyapata kaya hizo yakiwemo kuongezeka idadi ya wazazi na walezi wanaopeleka watoto kliniki, kaya kupata uwezo wa kununua chakula na mahitaji mengine tofauti na awali na baadhi yao kuanzisha miradi midogo midogo ya uzalishaji mali.
Alianisha baadhi ya changamoto zikiwemo upungufu wa magari unaopelekea shughuli hiyo kuchelewa lakini pia baadhi ya walengwa kutohudhuria wakati wa uhawilishaji fedha kutokana na kuhama, safari za mbali n.k. jambo lililopelekea asilimia mia kutofikiwa.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Selestine Gesimba aliwaasa Wajumbe wa kikao kujitahidi kuwasaidia walengwa hao ili hata mpango unapokoma basi waweze kuwa wamejikwamua. Alimaliza kwa mfano wa biblia wa mpanzi akisema, “mbegu imeshapandwa, sasa wajumbe tujihoji kama je, zimeanguka kwenye mwamba, kwenye magugu, kwenye miiba au udongo mzuri utakaowezesha mti kuzaa matunda?.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mkuu TASAF Bw. Zacharia
Ngoma alipongeza kasi ya Geita baada ya michango iliyotoka kwa waheshmiwa
wakuu wa Wilaya za Geita ambao pia walihudhulia akiamini kama viongozi wana
uelewa mzuri wa mpango huo, basi utafanikiwa; kisha kuwakumbusha kuzitembelea
kaya maskini vijijini ili kujifunza mengi zaidi.
Kikao
hicho pia kilihudhuriwa na Waratibu, Wahasibu na Maafisa Ufuatiliaji wa TASAF
ngazi ya Halmashauri na Wilaya bila kusahau Sekretarieti ya Mkoa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.