ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 11, 2018

WANASIASA WATOLEWA HOFU NA MKURUGENZI WA NEC


Mkurugenzi wa Tume ya Taifa Uchaguzi (Nec), Athuman Kiamia, amesema atavitendea haki vyama vyote vya siasa bila upendeleo wowote.

Amesema atahakikisha sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kuongoza Nec inafuatwa kwa uhalisia.

Aliyasema hayo jana kwenye mkutano baina ya Nec na viongozi wa vyama vya siasa, kuelekea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu, na madiwani kwenye kata 79 za Tanzania Bara unaotarajia kufanyika Agosti 12, mwaka huu.

“Tume inaongozwa na sheria, kanuni na miongozo kwa hiyo mimi Mkurugenzi wa Nec nitahakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa uhalisia wake, tutaendelea kuhakikisha haki inatendeka kwa makundi yote,” alisema Athumani.

Alisema pia atahakikisha anashirikiana na menejimenti ya Nec, wajumbe, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ili kila kitu kifanyike kwa wakati na haraka.

Athumani amechukua nafasi ya Ramadhan Kailima, aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Naibu Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kuhusu suala la mawakala, Mkurugenzi huyo mpya alisema Nec inatendelea kutoa elimu kwa vyama vya siasa kwa kuwa suala hilo limekuwa likileta mtafaruku mara kwa mara.

“Vyama vya siasa muhimu wazingatie muda wa uapishwaji, na uletwaji wa majina ya mawakala ufanyike siku saba kabla ya siku ya uchaguzi.”

“Wajibu wa mawakala na wasimamizi wa uchaguzi ukizingatiwa hakutakuwa na changamoto,” alisema Athumani.

Alisema kama alivyoweza kusimamia uchaguzi katika Jiji la Arusha alipokuwa Mkurugenzi kwa kusimamia kufanyika kwa uchaguzi mdogo marambili bila ya kuwapo kwa malalamiko.

Alisema atachanganya uzoefu alioupata katika Jiji la Arusha na maeneo mengine kuimarisha Nec.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Senistocles Kaijage, alisema Nec inatarajia kutumia Shilingi bilioni tatu kwenye uchaguzi huo.

"Bajeti iliyotengwa katika uchaguzi wa Jimbo la Buyungu na ule wa madiwani kwenye kata 79 ni bilioni tatu, fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia Julai 8 hadi 14, uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 14,  kampeni za uchaguzi zitaanza Julai 15 na kumalizika Agosti 11," alisema Jaji mstaafu Kaijage.

Kuhusu changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa marudio Jimbo la Kinondoni, Jaji mstaafu Kaijage alisema zilisababishwa na vyama vya siasa kutozingatia kanuni, taratibu na sheria zinazowaongoza.

Jaji Kaijage alisema wajibu wa kumtambulisha wakala au mawakala ni wasimamizi wa uchaguzi ambao wanawatambulisha kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.