Abu Sufian Qumu, aliyekuwa dereva mahsusi wa Usama bin Laden nchini Sudan |
Dereva wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Usama bin Laden ametiwa mbaroni katika mji wa Derna wa mashariki mwa Libya.
Taarifa hiyo imetangazwa mapema leo asubuhi na televisheni ya al Nahar al Jazayir ambayo imeongeza kuwa, askari wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar wamefanikiwa kumtia mbaroni Abu Sufian bin Qumu, aliyekuwa dereva wa Usama bin Laden katika jengo moja mjini Derna baada ya kundi lake kuishiwa na silaha wakati walipokuwa wanapigana na wanajeshi wa Khalifa Haftar.
Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na viongozi wa ngazi za juu wa al Qaida, bin Qumu ameshiriki pia katika vita vingi vya kundi hilo. Alikuwa dereva binafsi wa Bin Laden nchini Sudan.
Mwaka 2007 bin Qumu aliachiliwa huru kutoka jela ya Guantanamo na kutumikia kifungo chake nchini Libya, lakini alitoroka jela ya Abu Salim mwaka 2011 wakati wa kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi na kurejea katika mji wake alikozaliwa wa Derna, mashariki mwa Libya ambako alianzisha genge lenye misimamo mikali ya ukufurishaji la Ansar al Sharia.
Bin Qumu, 59, anahesabiwa kuwa mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa al Qaida ambaye alihamia Afghanistan baada ya kuacha shughuli zake za kawaida huko Libya katika miaka ya mwanzoni ya muongo wa 1980. Aliwasili Afghanistan kupitia Sudan na kupata mafunzo ya kigaidi katika kambi za al Qaida kabla ya kuwa mmoja wa viongozi muhimu wa mtandao huo aliyeshiriki katika vita vyake vingi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.