Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
YANGA SC imepata pointi ya kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya sare ya bila kufungana na Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa Kundi D uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo, Yanga inaendelea kushika mkia kwenye kundi hilo, nyuma U.S.M. Alger yenye pointi nne kileleni, Gor Mahia, Rayon pointi mbili kila moja baada ya mechi mbili za awali.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa kutoka Angola, Helder Martins De Carvalho aliyepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Ivanildo Meirelles De O Sanche Lopes na Wilson Valdmiro Ntyamba, kwa mara nyingine udhaifu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga uliiathiri timu.
Yanga ilikuwa inacheza vizuri kuanzia nyuma ikipitisha mashambulizi yake pembezoni mwa Yanga, lakini mipira kila ilipofika mbele ilichukuliwa na wachezaji wa Rayon kwa urahisi.
Winga chipukizi, Yusuph Mhilu ameendelea kuonyesha ubora wake kikosini Yanga, lakini nafasi zote alizotengeza hazikutumiwa vizuri na mshambuliaji Mzambia Obery Chirwa.
Dakika ya 83 Chirwa alikosa bao la wazi baada ya kugongesha mwamba wa juu kufuatia kazi nzuri ya Mhilu na hapo hapo kocha Nsajigwa Shadrack akamtoa na kumuingiza majeruhi wa muda mrefu, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe.
Mara mbili Rayon walitumbukiza mipira kwenye nyavu za Yanga, mara moja kila kipindi, lakini wakati walifanya hivyo kimakosa.
Kipindi cha kwanza mchezaji wa Rayon aliuchukua mpira uliotoka nje na kuutumbukiza nyavuni na kipindi cha pili mfungaji alikuwa amezidi.
Ikumbukwe mechi ya kwanza Yanga ilianza vibaya kwa kufungwa mabao 4-0 Mei 6 na U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, Algeria wakati Rayon ililazimishwa sare ya 1-1 na Gor Mahia siku hiyo mjini Kigali.
Michuano ya Kombe la Shirikisho inasimama sasa kupisha Fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi na Yanga watakamilisha mechi zao za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi katika makundi yote manne, zitakutana katika hatua ya Robo Fainali na baadaye Nusu Fainali itakayozaa Fainali.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko/Raphael Daudi dk66, Yusuph Mhilu, Pius Buswita, Obrey Chirwa/Amissi Tambwe dk84, Juma Mahadhi na Geofrey Mwashiuya/Emmanuel Martin dk88.
Rayon Sport; Eric Ndayishimiye, Gabriel Mugabo, Thierry Manzi, Mutsinzi Yannick, Shassir Nahimana, Sadam Nyandwi, Ismaila Diarra/Christ Mbonsi dk73, Pierre Kwizera, Mugisha Francois na Manishimwe Djabel/Kevin Muhire dk57.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.