CHANZO/MWANANCHI
Mbeya. Saa chache baada ya kutoka jela,
mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema ni
mfungwa wa kisiasa, “nilifungwa kiholela na nimetoka kiholela.”
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na
mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe leo Mei 10, 2018 walifika katika
Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya kuwapokea Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya
Nyasa, Emmanuel Masonga lakini walipigwa chenga ya mwili baada ya kuelezwa na askari
magereza kwamba wameshatoka, hivyo kulazimika kuwafuata nyumbani.
Akizungumza na MCL Digital leo Sugu
amesema, “Sikutaka kuhoji sababu za kutolewa, jana niliambiwa jiandae kesho
(leo) tutatoka, basi nasi tukasema haina shida kwa sababu sikuwa na sababu ya
kuwa ndani. Naamini sikutakiwa kuwa gerezani.”
Sugu akiwa na Masonga alifika nyumbani
kwake na kumkuta mlinzi pekee kutokana na mkewe Happiness Msonge kwenda Gereza
la Ruanda kuwapokea.
Dakika chache baadaye Happiness na mke
wa Masonga, Grace Malya walifika nyumbani hapo na kuwalaki kwa furaha huku
wakikumbatiana na kucheka.
Akizungumzia mazingira ya kuachiwa kwa
wawili hao, Mbowe amesema, “inaonyesha hawakuwa na sababu ya kuwepo gerezani
maana mazingira ya kutolewa kwao ni tata sana.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.