RAIS MAGUFULI AWAKABIDHI SIMBA KOMBE BAADA YA KUPIGWA 1-0 NA KAGERA SUGAR…AWAAMBIA; “KABORESHENI KIWANGO CHENU…KIMATAIFA BADO”
Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, John Pombe Joseph Magufuli amewakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Simba SC wakitoka kufungwa 1-0 na Kagera Sugar jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na kabla ya kuwakabidhi Kombe hilo, Rais Magufuli akawaambia Simba SC hajaridhishwa na kiwango cha mchezo wao na akawataka wakakiboreshe kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli amewapongeza Simb SC kwa kufikia kutwaa la ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mechi kabla ya kufungwa na Kagera leo.
Rais Dk. John Magufuli akimkabidhi Kombe Nahodha wa Simba SC, John Bocco leo
Wachezaji wa Simba SC wakifurahia na Kombe lao ubiongwa wa Ligi Kuu
“Mimi huwa ninafuatilia ligi mbalimbali, nilifuatilia hadi juzi timu ambazo zilikuwa zimechukua ubingwa bila kufungwa, zilikuwa zimebaki mbili, Barcelona na Simba, Jumapili iliyopita Barcelona wakafungwa na leo Simba nao wamefungwa,”alisema Rais Dk. Magufuli kabla ya kuwakabidhi Kombe hilo Simba SC.
Rais amesema kwamba anawapongeza Simba SC kwa sababu pia wamepitia kipindi kirefu bila kuchukua ubingwa na akasema anazipongeza na timu nyingine zilizoshiriki Ligi Kuu msimu huu huku akiwatania SImba; “Nashukuru hakuna timu iliyokwenda FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kudai pointi za mezani msimu huu,”.
Aidha, Rais Magufuli aliyewapongeza Kagera Sugar kwa kuonyesha mchezo mzuri leo pia alisema Simba SC nayo ilijitahidi na kudhihirisha wao ni mabingwa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa Florentina Zablon wa Dodoma aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Mashaka Mwandile wa Mbeya, bao pekee la Kagera Sugar limefungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Edward Christopher Shijja kwa kichwa dakika ya 84 akimalizia krosi ya Japhet Makalai kutoka upande wa kulia.
Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi akapoteza nafasi ya kuisawazishia Simba SC dakika ya nne ya muda wa nyongeza baada ya kukamilika kwa dakika 90 za kawaida kufuatia mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa Juma Kaseja.
Florentina Zablon aliwapa Simba penalti hiyo baada ya Okwi mwenyewe kuangushwa na kiungo mkongwe wa Kagera Sugar, George Kavilla.
Simba SC inabaki na pointi zake 68 baada ya kucheza mechi 29 na itakwenda mjini Songea kukamilisha msimu kwa kumenyana na wenyeji Maji Maji Mei 28 Uwanja wa Maji Maji. Kagera Sugar inafikisha pointi 34 katika mechi ya 29, ingawa wanabaki nafasi ya 10.
Kikosi cha SimbaSC kilikuwa; Said Mohamed Nduda, Nicholas Gyan/Muzamil Yassin dk46, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, James Kotei/Salim Mbonde dk50/John Bocco dk70, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco, Shiza Kichuya,
Kagera; Juma Kaseja, Suleiman Mangoma, Abdallah Mguhi, Juma Nyoso, Mohamed Fakhi, Peter Mwalyanzi, Japhet Makalai, Ally Ramadhani/George Kavilla dk58, Japhery Kibaya/Paul Ngalyoma dk79, Edward Christopher, Atupele Jackson/Omar Daga dk32.
PICHA ZOTE NA BINZUBEIR
PICHA ZOTE NA BINZUBEIR
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.