ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, May 28, 2018

JAMII YATAMBUA UMUHIMU WA MWANAMKE KUMILIKI ARDHI.

Wananchi wa Kijiji cha Mawala, Wilaya ya Kilolo Iringa, wakisaidia kutekeleza baadhi ya shughuli za mpango wa matumzi ya ardhi ya kijiji chao.
Bahati Mwinyimvua mwananchi toka kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero Morogoro. Akichangia hoja kuhusiana na umiliki wa ardhi kwa wanawake
Ng’eng’enu Mambega katibu wa kamati ya maamuzi kijiji cha Mela, wilaya ya Mvomero Morogoro akibainisha jinsi elimu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake ulivyosaidia kuwabadili kifikra na kuwapa wenza wao maeneo wayamiliki. 
Angolile Rayson Afisa mradi toka Shirika la PELUM Tanzania akichangia mada kuhusiana na mpango wa matumzi ya ardhi.Jamii kwa sasa imeanza kutambua na kuthamini haki za mwanamke kwenye masuala ya umiliki wa ardhi na hivyo kumpa nafasi zaidi kisheria kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa wanaume. 

Kuwepo kwa mabadiliko haya chanya kwa baadhi ya jamii imetokana na kusambaa kwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika kusimamia sekta ya kilimo unaofadhiliwa na watu wa marekani. 

Angolile Rayson ambaye ni Afisa Mradi amesema vijiji vyote 30 vya mradi ambavyo 27 kati yake toka wilaya sita za Morogoro, Mvomero, Kilolo, Mufundi, Bahi na Kongwa vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi, wananachi wake walikuwa wakiendeleza mila na tamaduni potofu za kuona kuwa mwanamke si sehemu ya familia hivyo hapaswi kumiliki ardhi kwani ataolewa na kwenda kuendeleza ukoo mwingine. 

Lakini baada ya kufanya mafunzo kwenye vijiji hivyo juu ya haki za mwanamke kumiliki ardhi, jamii imebadilika na sasa mwanamke si tu amekuwa akimilikishwa ardhi peke yake bali pia ana maamuzi nayo kisheria kuitumia kwa shughuli zozote za kiuchumi, kukodisha na hata akiamua kuiuza. 

“Tunashukuru baada ya kutoa elimu juu ya haki za mwanamke kumiliki ardhi wakati wa kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi, wanaume wengi wamewapa wenza wao maeneo wamiliki kwa majina yao wenyewe na wengine wamemiliki umiliki wa pamoja yaani mke na mume na zaidi ya yote hata watoto wa kike kwenye baadhi ya familia wamepewa maeneo na wazazi wao wamiliki. Shirika kupitia Hamlashauri za wilaya husika tumewapimia maeneo yao na kwa sasa wanasubiri hatimiliki za kimila ili wawe na umiliki halali jambo ambalo sisi kama Shirika tumeona ni sehemu kubwa ya mafanikio.” Alifafanua Angolile 

Wakielezea wakati wa kufanyika tathimini ya mradi wananchi wa kijiji cha Ikuka Wilaya ya Kilolo, Iringa walibainisha kuwa katika kijiji chao hapakuwa na mazingira mazuri hasa upande wa wanawake na watoto wa kike wanapoomba kupewa ama kurithishwa ardhi kilichokuwa kinafuata ni muhusika kufariki katika mazingira tatanishi hali iliyowafanya wahusishe suala hilo na imani za kiushirikina 

Kutokana na hali hiyo, wanawake iliwapasa kutokuzungumzia neno ardhi midomoni mwao. Ila baada ya kupata elimu, kwa sasa wanawake wamepimiwa vipande vya ardhi walivyopewa na wenza wao ikiwemo wengine kuwa na umiliki wa pamoja wa mume na mke. 

“Tunashukuru Shirika la PELUM Tanzania kwa kutupa mafunzo ya haki za ardhi ambayo yamekuwa msaada na hasa kwa wanawake kwani kupitia elimu hii tumefahamu haki zetu kama wanawake kuwa na sisi tunapaswa kumiliki ardhi na kuwa na maamuzi nayo kisheria. Kwenye kijiji chetu kwa sasa wapo wanawake wamepima ardhi zao mmoja mmoja na wengine wanatarajia kuwa na umiliki wa mume na mke kama mimi na sasa tunasubiri ugawaji wa hatimiliki.”Bahati Mwinyimvua Mwananchi kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoro. 

Ng’eng’enu Mambega yeye ni katibu kamati ya maamuzi kijiji cha Mela, wilaya ya Mvomero Morogoro anasema baada ya kupata elimu ya masuala ya ardhi kwa sasa si tu wamewapa maeneo wenza wao wayamiliki ambao yameshapimwa kupitia mradi ila pia wanawashirikisha mambo mbalimbali wenza wao na kuwaruhusu kufanya maamuzi jambo ambalo halikuwa likifanyika kweye tamaduni za kimasai. 

“ Zamani tulikuwa tunawathamini na kuwarithisha watoto wa kiume ardhi hata kama mzee kafariki kijana ndio anakuwa mwenye sauti lakini kwa sasa mambo yamebadiliki mama naye ana haki zake kwenye eneo la mume wake na vijana wa kike pia tumewapa maeneo wayamiliki wenyewe.” Alifafanua Mambega 

Kwa upande wake Zaveria Mdendemi toka kijiji cha Makungu, Wilaya ya Mufindi Iringa anasema, kutokana na mila potofu kuwa mwanaume ama mtoto wa kiume pekee ndio anapaswa kumiliki ardhi, jambo lilimletea mgogoro na mtoto wake wa kwanza wa kiume ambaye alitaka kumpokonywa mali zote ikiwemo ardhi aliyoachiwa na marehemu mume wake lakini kupitia elimu aliyoipata, alimpeleka kwa mwenyekiti wa kijiji akaeleimishwa na hatimaye akamuachia mama yake mali zote akisubiri maamuzi ya mama juu ya mali hizo. 

“Nashukuru mradi huu kutoa kipamumbe kwa wajane kupimiwa maeneo yao, kwani mila na desturi ambazo tumezikuta mwanamke amekuwa akinyimwa nafasi kumiliki mali yoyote na hasa sisi wajane pindi mume anapofariki tumekuwa tukifukuzwa kwenye nyumba tulizojenga na wenza wetu na kupokonywa mali zote wakati mwingine hadi watoto ama uachiwe watoto bila mali yoyote. Lakini kwa sasa elimu imewezesha jamii kutambua thamani ya mwanamke kumiliki ardhi na hivyo tumefanikiwa kupimiwa maeneo yaliyobaki mikononi mwetu”. Rosemary Ulanga mwananchi kijiji cha Ibugule, wilya ya Bahi Dododma. 

Kupitia upimaji huo wa ardhi kwenye vijiji 27, Shirika la PELUM Tanzania linatarajia kutoa hatimiliki za kimila zipatazo 4000 kwa makundi ya wazee, wajane, wagane, watu wenye ulemavu na wa kipato cha chini

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.