ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, April 17, 2018

WAJUMBE BODI YA SHULE YA THAQAAFA, UONGOZI WA MSIKITI WA IJUMAA WALIAMUSHA DUDE TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZIO.

Sherally.
NA PETER FABIAN, MWANZA.
WAJUMBE wanne Waasisi wa Bodi ya Shule ya Thaqaafa kwa kushirikiana na Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa (Sheikh Amin) Mjini Kati jijini Mwanza  wameliamusha ‘Dude’ kudai taarifa za Mapato na Matumizi ya Shule hiyo sanjari na kufungua kesi mahamakani kuishitaki Bodi hiyo kwa ubadhirifu, uendeshaji mbaya, ukiukwaji wa mambo mbalimbali ikiwemo Katiba Taasisi hiyo.

Baadhi yao wakizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari juzi wajumbe hao Abdallah Amin Abdallah, Bihoga A. Bihoga Sheikh Jabir Yusuf Katura, Miraji Mbwana na Sherally Hussein Sherally walieleza kuwa viongozi wakuu ambao ni Mwenyekiti wa Bodi na Katibu  wa Shule hiyo wamekaidi matakwa ya wajumbe ya kufuata Katiba iliyowaweka madarakani na kujiendeshe kinyume na taratibu na sheria.

Wamebaini kuwa viongozi hao wamekuwa wakikopa kwenye Taasisi za fedha (Benki) mbalimbali bila idhini ya Bodi na haifahamiki kiasi gani wamekopa hadi sasa, dhamana iliyowekwa dhidi ya mikopo hiyo, italipwaje na fedha hiyo ilifanya kazi gani tangu shule imeanzishwa miaka zaidi ya 22 iliyopita.

“Mwenyekiti na Katibu kwa ushirikiano na Menejimenti (Utawala) wanaingiza mali, vifaa na magari kutoka nje ya nchi  kwa jina Bodi ya Wadhamini na wamekuwa wakisamehewa Kodi na Serikali bila ridhaa ya wadhamini wote, kibaya zaidi mali hizo hazijulikani zilipo.Pia wameshindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa zaidi ya miaka 25(muda mrefu) na hivyo kukiuka Katiba,”alisema  Sherally wakati akisoma taarifa yao.

Sherally alisema Katibu wa Bodi ya Shule hiyo (hakumtaja) alitumia ubabe na mbinu chafu kuwaondoa baadhi ya wajumbe waasisi wa Bodi ya Shule ya Thaqaafa kinyume na taratibu, kanuni na sheria kwa madai ya kuwafukuza bila kujali hadhi na heshima yao kwenye jamii na kuwaweka mtoto wake na ndugu wa familia.

Taarifa hiyo ilizidi kueleza kuwa viongozi hao walibadilisha Namba ya Utambulisho Mlipa Kodi (TIN) 107 331568 iliyokuwa ikisomeka kwa jina la The Registered Trustee of Thaqaafa na kusomeka The Registered Trustees of Thaqaafa Foundation ambapo  pia walianzisha TIN nyingine Namba 101 027201 kwa jina la Thaqaafa Secondary School bila idhini ya Wajumbe wa Bodi (Without Board Resolution).

“Kuna mikataba  mingi imeingiwa na viongozi hao tangu kuanzishwa kwa Shule hiyo, Ujenzi unaohitaji malipo makubwa bila kupata ridhaa halali ya Bodi na hata baadhi ya zabuni wanapeana kifamilia na kutolewa kwa ujanja ujanja. Bodi ya Thaaqafa imewekeza kuendesha Zahanati ya Msikiti wa Ijumaa kwa thamani ya Sh. bilioni 1.5, fedha hizo hazijulikani zimetoka wapi,”

“Bodi ya Wadhamini na Uongozi wa Msikiti haijui faida inayopatikana kutoka kwenye Zahanati hiyo na uendeshaji wake Bodi halali ya Thaqaafa haina taarifa tangu ilipokodishiwa kwa Thaqaafa. Pia tumebaini Manunuzi yanafanyika chini ya mikono ya wajumbe wawili wa Bodi tu,”alisema Sherally.

Alisisitiza kuwa kwa uzito wa suala hili ikiwemo Taasisi moja kuwa na TIN mbili kwa majina tofauti,  ni vyama ikachunguzwa na Taasisi husika na ifahamike  kuwa baadhi Wajumbe wa Bodi hatuhusiki na madhambi hayo yaliyofanywa na viongozi wachache kwa tama zao na ndio maana tunakamilisha taratibu za kufungua kesi na kwenda mahakamani kutafuta haki ya waumini wa Msikiti wa Ijumaa .

“Baadhi yetu ambao ni waasisi wa Taasisi hii na ni wajumbe wa bodi hai ya Thaaqafa tumeamua kulipeleka suala hili  mahakamani.Tutafungua kesi ya msingi, kuiomba mahakama iwalazimishe viongozi waandamizi wa shule ya Thaaqafa watoe taarifa zote zinazohitajiwa na wajumbe na pia wafuate katiba ya taasisi na sheria za nchi kwa kuwa mali hizo ni za Waislamu wa Msikiti wa Ijumaa,”alisema Sherally.

 Awali Katibu wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya shule hiyo Abdallah Amin alisema hakubaliani kuona watu wachache wanajimilikisha na kunufaika na mali za Waislamu wa msikiti huo na wamefarijika kutokana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kuwataka waliohodhi na kujimilikisha mali za Waislamu wazirejeshe.

Meneja wa Shule ya Thaaqafa Maruzuku Magongo ambaye pia ni  Katibu wa Bodi ya shule hiyo alipotakiwa na waandishi wa habari kuzungumzia suala hilo alikiri kuwa shule hiyo ni mali ya Waislamu na kutuma ujumbe mfupi sms kwa simu ya mkononi kwa madai kuwa habari hizo niza uongo zinalenga kumchafua tu hana tatizo lolote juu ya shutuma na madai hayo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.