Kampuni ya Star Media (T) Ltd yenye chapa ya StarTimes pamoja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano mjini Dodoma. Mkataba huo Mpya utasaidia Kampuni zote mbili kunufaika na ushirikiano huo.
Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa huu utakuwa ni ukurasa mpya kwa pande zote mbili, “kama alivyosema Waziri Mkuu nina matumaini makubwa sana na Ushirikiano huu, kwa sababu kupitia Ushirikiano huu ndio tutaona TBC ikipanda kiteknolojia, ikipanda kivifaa na ikipanda kwa weledi”, alisema Waziri Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe pia alizungumzia kwa upande wa wizara na nafasi yake, “Ni wajibu wa Wizara kuhakikisha yote tuliyokubaliana yanatekelezwa”. Akizungumzia mkataba huo Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Dk. Ayoub Rioba amesema kasoro zilizokuwepo awali sasa zimeondoshwa ili kuanza ukurasa Mpya na yeye kwa upande wake atakuwa Mwenyekiti wa Bodi huku TBC ikimiliki asilimia thelathini na tano (35%).
“Makubaliano haya ambayo tumesainiana leo ni kuondoka kule ambako tumekuwa twende katika muktadha mpya, ambapo Kampuni itaendeshwa kwa uangalizi wa karibu sana, watanzania na mimi kama Mwenyekiti wa bodi tumeshaanza kuanzia hivi ninavyozungumza kuna namna tunafanya mambo tofauti ili tuhakikishe tunasimamia vizuri hiyo Kampuni”.
Prof. Rioba pia alizungumzia upiaji upya wa mikataba ili kuondoa kasoro za awali, “moja ya makubaliano ni kwamba tutapitia upya Mkataba na tumeshaanza, wao wameshaona mambo ambayo yana kasoro kwa upande wao sisi pia tumeona kwa upande wetu na wote tumeyajadili tumeona kuna kukubaliana kwa hiyo kinachofuata tunaangalia upya ule mkataba wa Ubia ili zile kasoro nyingine za msingi ambazo zilisababisha uendeshaji haukuwa mzuri tunaziondoa ili tuende katika namna ambayo hatutarudia tena kuwa na matatizo ambayo tumekuwa nayo”.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.