ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 13, 2018

MGOGORO MWAKITOLYO KUPATIWA UFUMBUZI

 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo Wilayani Shinyanga (hawapo pichani) kuhusu mgogoro wao na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
 Wananchi wa Kijiji cha Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) akizungumza kuhusu mgogoro wao na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
 Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum akizungumza na wananchi wake wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani Shinyanga kuhusiana na mgogoro wao na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akijadiliana jambo na mwenyeji wake Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum wakati wa mkutano na wananchi wa Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga wa kujadili mgogoro wao na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
 Mkuu wa Wilaya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga wakati wa mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hauypo pichani).
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum (anayemfuatia) wakisikiliza kero za wananchi wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani Shinyanga kuhusiana na mgogoro wao na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.

MGOGORO MWAKITOLYO KUPATIWA UFUMBUZI

Wananchi wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani Shinyanga wametakiwa kufanya subira wakati mgogoro wao wa fidia na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji madini ya Henan Afro Asian Engineering ukitafutiwa ufumbuzi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa wito huo Machi 12, 2018 kwenye mkutano na wananchi hao uliofanyikia kwenye Kitongoji cha Mahiga na kuhudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Serikali.

Mkutano huo unafuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alilolitoa Machi 11, 2018 kwenye mkutano na wananchi wa Kahama ambapo alielezwa na Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum kuwa wananchi wa Mahiga wana mgogoro wa muda mrefu na mwekezaji hususan kuhusiana na suala la ulipaji fidia ili kupisha mradi.

Kufuatia maelezo hayo ya Mbunge, Rais Dkt. Magufuli alimuagiza Naibu Waziri Biteko kuhakikisha anafika kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi na kuwasikiliza wananchi. 

Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni wakati sasa Watanzania waanze kunufaika na rasilimali zao ikiwemo madini. "Tunataka madini yawanufaishe Watanzania," alisema Rais Magufuli.

Alisema wawekezaji wakifika nchini ni lazima wahakikishe Watanzania wananufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira, kodi na tozo.

"Jukumu langu nimeamua kusimamia suala hili; Nawahakikishia Serikali iko imara kwa ajili ya kuwatetea wanyonge," alisema Rais Dkt. Magufuli.

Aliagiza mwekezaji atakayehitaji kuchimba kwenye maeneo yenye wachimbaji wadogo ni lazima kwanza akubaliane nao ikiwemo suala la ulipaji wa fidia na sio kuwafukuza.

"Suala la wachimbaji lizingatiwe kwa mujibu wa sheria. Tuwalee ndio maana tumeanzisha vituo vya mfano maeneo mbalimbali ili wajifunze," alisema.

Aidha, kwa mujibu wa Mbunge huyo ni kwamba mgogoro huo ulianza tangu Julai 2017 baada ya mwekezaji huyo kuanza shughuli zake za kuandaa mazingira ya kuchimba bila kuwa na makubaliano maalum na wananchi hao.

Akiwa katika mkutano na wananchi hao, Biteko alielezwa kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kutoridhishwa na kiasi cha fidia kilicholipwa ili kupisha maeneo yao kwa ajili ya mwekezaji, wengine kutohitaji kabisa fidia na maombi ya baadhi yao kuruhusiwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na uchimbaji kwenye maeneo husika.

Biteko aliwataka kufanya subira wakati Serikali inatazama namna bora ya utatuzi wa hoja zao kwa mujibu wa sheria ili manufaa yapatikane bila kumuonea yoyote.

Alisema Rais Dkt. John Magufuli anataka kuona Watanzania wanyonge wananufaika na rasilimali zao ikiwemo rasilimali madini.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ni Serikali inayowaangalia wanyonge. Nimesikiliza kero zenu nitazifikisha na hatua itachukuliwa kwa mujibu wa sheria. Mfanye subira," alisema Biteko

Aliongeza kuwa Serikali haipo tayari kuona Watanzania wanyonge wanateseka na kwamba wakati umefika wa wao kunufaika.

Alifafanua kuwa suala lao litashughulikiwa kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria ili haki itendeke pasipo kumuumiza yoyote.

Hata hivyo aliwakumbusha wananchi hao kuhakikisha wanafuata utaratibu na sheria ili manufaa yapatikane bila kuleta madhara yoyote.

Aidha, kwa mujibu wa Mthamini wa Wilaya ya Shinyanga, Devotha Njella ni kwamba wananchi waliofanyiwa tathmini ni 500 na kwamba bado mwananchi mmoja mwenye heka 25 na nyumba 6 ambaye alikataa.

Alifafanua kwamba malipo hayo ya fidia yalifanyika kwa awamu mbili na kwamba katika awamu ya kwanza Shilingi 953,194,050.75 zililipwa na awamu ya pili kiasi kilicholipwa ni Shilingi 472,413,686.32 na kwamba bado kiasi cha Shilingi 208,886,951.01 ambacho taratibu za kulipa zinaendelea.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.