Wananchi mkoani Mwanza wametakiwa kutoa ushirikiano wa dhati kwenye zoezi la Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa mwaka 2018/19 unaondelea katika maeneo mbalimbali.
Katibu Tawala mkoani Mwanza, Clodwin Mtweve ametoa rai hiyo leo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Mwanza John Mongella, wakati wa utoaji wa taarifa ya zoezi la utafiti huo kwa vyombo vya habari.
Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoani Mwanza, Goodluck Lyimo alisema zoezi la utafiti huo linahusika jumla ya kaya 408 mkoani Mwanza ambapo tayari Kaya 68 zimekamilisha mahojiano, Kaya 30 zinaendelea na mahojiano na kwamba hadi kufikia februari 28 mwaka huu Kaya 98 zitakuwa zimekamilisha mahojiano hayo.
Afisa habari kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Emmanuel Gulla alibainisha kwamba utafiti huo ni wa saba kufanyika nchini tangu uhuru na kwamba utafiki wa mwisho ulifanyika mwaka 2011/12 na kuonyesha kuwa asilimia 28.2 ya watanzania wanaishi chini ya mahitaji ya msingi.
Afisa Masoko Mhamasishaji wa Mapato na Matumizi ya Kaya kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Andrew Punjila alisema ni muhimu wananchi wataohojiwa kwenye utafiti huo, wakatoa taarifa sahihi ili kuisaidia serikali kutambua hali ya wananchi wake pamoja na upangaji wa mipango ya taifa ya maendeleo.
Wananchi wanakumbushwa kwamba utafiti wa aina hii ni muhimu katika taifa kwa ajili ya kuisaidia serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kutathimini hatua stahiki katika kutimiza malengo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yakiwemo mpango wa pili wa taifa wa maendeleo pamoja na mpango wa maendeleo endelevu wa mwaka 2030.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.