Aidha, imeeleza mvua hizo zinasababishwa na kimbunga ‘Alva’ ambacho kinatoka eneo la Mashariki mwa kituo cha Madagascar kuanzia Januari 3, mwaka huu na kuongeza unyevunyevu pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa Bahari ya Hindi.
TMA imesema mikoa inayopitiwa na mvua hizo ni ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini ikiwamo Pwani, Tanga, Dar es Salaam na iliyopo ukanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, ikiwamo Manyara, Kilimanjaro na Arusha.
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha TMA, Samuel Mbuya, aliiambia Nipashe jana kuwa tahadhari inapaswa kuchukuliwa kwa wasafiri katika Bahari ya Hindi kwa kuwa mwezi wa Januari kuna hali ya joto la bahari eneo la Magharibi kuathiri ukanda huo.
“Kwa kipindi cha Januari mwaka huu mvua hizi zitaendelea ambazo zipo nje ya msimu, Dar es Salaam ikiwamo, hii ni kutokana na joto la Bahari ya Hindi katika eneo la Magharibi,” alisema Mbuya.
Pia katika mikoa ya ukanda wa kati Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma Katavi, Rukwa na Nyanda za Juu Kusini Mashariki, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma na Mtwara yataendelea kupata mvua za msimu hadi mwezi ujao.
Mvua zilizoanza kunyesha mwishoni mwa wiki kanda ya Pwani ikiwamo jijini Dar es Salaam, zilisababisha athari katika maeneo kadhaa ikiwamo wananchi kukosa makazi na kusitishwa kwa muda kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka, maarufu mwendokasi.
Wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni ni kati ya waathiriwa hao kutokana na mvua kuzingira makazi huku barabara kadhaa zikijaa maji kutokana na mitaro na kusababisha msongamano wa magari
kwa waliokuwa wanakwenda kazini, sehemu za biashara, maeneo mengine na wanafunzi waliokuwa wanakwenda shuleni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika, katika taarifa yake juzi aliwataka wakazi wa mabondeni kuhama mara moja bila kusubiri kukumbwa na mafuriko.
“Badala ya kuendelea kuishi katika maeneo hatarishi wakisubiri kuondolewa na serikali, wahame haraka kunusuru maisha yao na wasirudi tena katika maeneo hayo,” alisema Kitalika.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.