ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 2, 2017

WATOTO 1,300 WALIOPOTEA POLISI WAANDA KUWASAKA.


JESHI la Polisi mkoani Pwani, limesema limeanza kuwasaka wanafunzi 1,300 wanaodaiwa kutoweka wilayani Kibiti.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya gazeti dada la hili la MTANZANIA kumnukuu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, akisema kuwa taarifa za kutoonekana kwa watoto hao zimetoka Idara ya Elimu na Wazazi.

IGP Sirro ambaye alizungumzia suala hilo alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani mapema wiki hii, hata baadaye alipozungumza na chumba hiki cha habari alisisitiza kuwa

“Kama mtoto humwoni shuleni wala nyumbani ni lazima uripoti.”

Jana MTANZANIA Jumamosi, lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shana, ambaye alisema msako wa watoto hao utafanywa kwa kushirikiana na walimu pamoja na wazazi wao.

Kamanda Shana pamoja na kuwataka baadhi ya watu kupingana na hisia kwamba watoto hao wamejiunga na vikundi vya kigaidi, alisisitiza kuwa Jeshi la polisi litakuja na majibu sahihi kuhusu mahali walipo watoto hao.

“Tumekubaliana kufanya operesheni ili kuhakikisha watoto hao wanapatikana, taarifa hii inashtusha kwa kuwa wapo watu ambao wanahusisha kupotea kwa watoto hao na ugaidi, wanadhani wamejiingiza katika vikundi hivyo jambo ambalo si kweli,” alisema Kamanda Shana.

Alisema operesheni hiyo pia itawagusa watoto ambao wanashindwa kuhudhuria masomo yao kwa sababu  ya mashinikizo ya wazazi ikiwemo kuwafanyisha kazi za nyumbani.

“Watoto ambao hawaendi shule tumepanga kushirikiana na walimu kupita nyumba hadi nyumba kuhakikisha tunawashurutisha wazazi kuwaamrisha watoto wao waende shule kama sheria inavyotaka, sheria ipo wazi katika hilo,” alisema Shana.

Taarifa za kupotea kwa watoto hao katika kipindi cha kati ya mwaka 2016 na Julai mwaka huu, zilipatikana juzi wakati IGP Sirro alipofanya ziara ya kikazi wilayani Kibaha, Pwani.

Katika ziara hiyo, IGP Sirro alizungumza na wazazi, walimu, viongozi wa mashirika ya umma, wazee maarufu, wastaafu mbalimbali na kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani kuhusu taarifa hizo.

Kupitia mkutano huo, IGP Sirro, alieleza taarifa ya wanafunzi zaidi ya 1,300 mkoani humo ambao hadi sasa hawajulikani walipo na hawajaonekana shule wala katika familia zao.

IGP Sirro alisema huenda watoto hao ni watoro, hivyo aliwataka wazazi washirikiane na Jeshi la Polisi kujua walipo.

Pia aliwataka wazazi kusaidiana na walimu wa shule za msingi na sekondari, ambazo wanafunzi walikuwa ni watoro ama hawajaripoti shule kwa miezi kadhaa, kutoa taarifa kwani wapo baadhi ya watoto wanaotumika kufundishwa uhalifu hata wa kutumia silaha na watu wasio wema.

Kutokana na utata wa taarifa hizo, gazeti la MTANZANIA la jana lilizungumza na IGP Sirro, ambaye alisema taarifa za kutoonekana kwa watoto hao zinatokana na Idara ya Elimu na wazazi.

“Ni taarifa ya muda mrefu, kipindi cha mwaka jana na mwaka huu, ni zaidi ya mwaka mmoja niliipata Wizara ya Elimu kule, ndiyo maana nimeelekeza wazazi ambao hawawaoni watoto wao kutoa taarifa.

Hadi sasa haijaelezwa wanafunzi hao waliopotea ni wa shule za msingi au sekondari.

Taarifa hizo zimekuja katika wakati ambao hali ya usalama katika wilaya ya Kibiti na Rufiji imeimarika tofauti na miezi kadhaa iliyopita, lilipoibuka kundi la wahalifu ambao walikuwa wakiua watu wakiwamo askari polisi.

Mauaji yaliyotikisa wilayani humo yalisababisha si tu hofu bali baadhi ya watendaji kukimbia vituo vyao vya kazi.

Hivi karibuni IGP Sirro alisema hali ya usalama imerejea katika maeneo hayo yaliyokumbwa na mauaji na zaidi alisisitiza kuwa wahalifu waliokuwa wakitekeleza vitendo hivyo vya kinyama wamekimbilia katika nchi jirani ya Msumbiji.

Chanzo Mtanzania

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.