ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, November 10, 2017

TAKUKURU YAVIONYA VYAMA VYA SIASA KUHUSU RUSHWA.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imevionya vyama vya siasa na washirika wao, wakiwemo wagombea katika uchaguzi mdogo wa madiwani kuhusu kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Ofisa wa Takukuru Wilaya ya Arusha, Jacqueline Kapileh ametoa onyo hilo akitoa mada kwenye baraza la madiwani jana Alhamisi 9,2017.

Uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika katika kata 43 nchini Novemba 26,2017 na kati ya hizo nane ni za Mkoa wa Arusha ambazo ziko wazi kutokana na waliokuwa madiwani kujiondoa Chadema na baadhi kujiunga na CCM.

Kapileh amesema hatua za kisheria zitachukua mkondo wake kwa watakaobainika kujihusisha na rushwa na hasa katika kipindi hiki cha kampeni.

"Tutahudhuria mikutano yote ya kampeni na wengine tutaweka makazi sehemu zinazoendeshwa uchaguzi ili kubaini kwa ukaribu vitendo hivi, na hasa wale washirika wa vyama na wagombea wanaowasumbua wananchi na kuwashawishi kuwapatia rushwa kuwachagua," alisema.

Pia, amewaonya wananchi wenye tabia ya kuwashawishi wagombea kuwapatia rushwa ili wawafanyie kampeni au kuwapigia kura.

Amesema Taifa haliwezi kuwa na kiongozi aliyeshinda kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa wanategemea viongozi wanaopita katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wawe sehemu ya kutekeleza maagizo ya Serikali kwa masilahi ya wananchi ikiwemo kupiga vita rushwa.

Diwani wa Viti Maalumu katika Kata ya Ngarenaro, Happy Challe ameiomba Takukuru kutoa onyo kwa CCM kuondoa picha za wagombea kwenye miradi ya Serikali inayotekelezwa na hasa kwenye kata zenye uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia amesema, "Lengo la uchaguzi ni kupata wawakilishi wa Serikali, hivyo lazima apatikane kwa mapenzi ya wananchi. Nitasimamia utekelezaji na kutokomeza vitendo vyote vitakavyoashiria kuharibu uchaguzi."

Mkazi wa Kata ya Muriet ambako kutafanyika uchaguzi mdogo wa udiwani, Neema Marko ameiomba Serikali kudumisha ulinzi katika eneo lao kutokana na baadhi ya washirika wa vyama kuwasumbua na hasa usiku kuwaomba kura huku wakitoa vitisho kuwa wasipowachagua watacheleweshewa maendeleo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.