ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, September 12, 2017

POLISI WAKANUSHA ASKARI WAKE KUMFUATILIA MBUNGE LISSU KENYA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI JESHI LA POLISI TANZANIA



Anuani ya Simu “MKUUPOLISI”
Ofisi ya Inspekta  Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734
Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 21355
S.L.P. 9141,

DAR ES SALAAM.





12/09/2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika siku za karibuni kumejitokeza vitendo vya baadhi ya watu kutumia majina ama picha za watu na kuwahusisha na matukio ya kihalifu au matukio yanayohusiana na uhalifu kwa lengo la kujipatia umaarufu, kuwachafua watu hao au kuwakosanisha na jamii inayowazunguka.

Mnamo tarehe 11.09.2017 kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa picha ya askari wa Jeshi la Polisi akihusishwa na muendelezo wa tukio la kujeruhiwa kwa risasi kwa Mhe. Tundu Lissu (MB) ambapo taarifa hiyo ilimtambulisha askari huyo kuwa ni kachero wa Kitengo cha Interpol na kwamba yupo jijini Nairobi nchini Kenya akifuatilia taarifa za Mhe. Lissu.

Jeshi la Polisi linapenda kukanusha taarifa hizo kuwa si za kweli na ni za uongo zenye lengo la kumchafua askari huyo na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Askari huyo hayupo Nairobi kama ilivyoenezwa na picha iliyotumika ilipigwa hapa nchini tarehe 07.01.2017 kwenye sherehe ya mahafali ya mtoto wa kaka yake.

Kuhusiana na safari ya Nairobi, askari huyo alikuwa nchini Kenya kwa kozi ya kimafunzo kuanzia tarehe 04.09.2017 na kurejea tarehe 08.09.2017, huku Mhe. Lissu akipatwa na mkasa wa kujeruhiwa kwa risasi Tarehe 07.09.2017 na kusafirishwa kwenda Nairobi usiku wa kuamkia tarehe 08.09.2017.

Jeshi la Polisi linakemea vikali kitendo hiki chenye lengo la kumharibia maisha yake askari wetu, na linawataka wale wote waliohusika kusambaza au kutajwa katika taarifa hizo kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano. Vilevile tunatoa onyo kwa wote wanaofikiri kuwa wanaweza kukaa na kupika habari ili waweze kuivuta jamii iwe upande wao na kuchafua upande wa serikali.

Suala hili la Mhe. Lissu lipo chini ya uchunguzi ili kuwabaini wote waliohusika na tukio hili na hatimaye kuwafikisha mahakamani. Ni vema wananchi na wanasiasa wakaliacha Jeshi la Polisi liweze kufanya kazi yake bila kuliingilia ili kuweza kupata ukweli wa jambo hili.

Jamii itambue kuwa Jeshi la Polisi linafanyakazi kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za Nchi na kamwe halifanyi kazi kwa kuvizia. Endapo mtu yeyote anahitaji taarifa, tunayo mifumo yetu rasmi inayotuwezesha kupata taarifa tuzitakazo kupitia uhusiano tulionao ndani na nje ya nchi.

Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha upelelezi wa makosi ya mitandao (Cyber Crime Investigation Unit) linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wote waliohusika na kusambaa kwa taarifa hizi za uongo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya na badala yake mitandao hii itumike kwa ajili ya kuelimisha na kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya kimaendeleo.






Imetolewa na:
Barnabas David Mwakalukwa - ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi

Makao Makuu ya Polisi.


www.policeforce.go.tz         www.twitter.com/tanpol            www.facebook.com/tanpol    www.usalama2.blogspot.com

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.