ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, August 17, 2017

HAYA NDIYO YALIYOJIRI KWENYE MKUTANO WA KWANZA MARA BAADA YA KUSHINDA KESI MBUNGE WA JIMBO LA BUNDA MHE. ESTER BULAYA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitikisa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, baada ya kufanya mkutano mkubwa wa hadhara, huku mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, akitangaza kutoa sh. milioni 20 kwa ajili ya kutatua kero ya maji jimboni humo.

Aidha, mwanasiasa huyo ametangaza kuwafungulia kesi ya madai ya mamilioni ya fedha wapinzani wake waliokuwa wakipinga ushindi wake mahakamani, baada ya 'kuwagaragaza' katika Mahakama ya Rufani nchini.


Bulaya alitangaza hayo juzi alipohutubia mkutano wake wa hadhara uliofanyika Stendi ya Mabasi ya zamani mjini hapa, ambapo aliahidi pia kulisaidia Jeshi la Polisi Wilaya ya Bunda, gari la doria kwa ajili ya kupambana na wahalifu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa (Zanzibar), Salum Mwalim, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Joyce Sokombi, Katibu wa Chadema mkoa huo, Chacha Heche na madiwani wa chama hicho.

Bulaya alisema licha ya kufungiwa kuhudhuria vikao bungeni kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kile alichosema ni njama za CCM, kamwe hatakata tamaa kupeleka maendeleo ikiwamo utatuzi wa kero ya maji jimboni humo.

"Nimewamis (akashangiliwa). Hata wakinifukuza bungeni miaka miwili sitaogopa wala kunyamazishwa. Nasema sitawaangusha wananchi wangu wa Bunda. Mimi nina hoja, sina vioja (akashangiliwa tena).

"Nitatoa sh. milioni 20 kwenye Mfuko wangu wa Jimbo kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa maji, kata saba za jimbo hili," alisema Bulaya aliyekuwa akishangiliwa mara kwa mara na umati wa watu uliokuwa umejaa mkutanoni hapo na kuongeza:

"Kwani Spika wa Bunge aliyetangaza kunifungia si anatoka CCM?" alihoji Bulaya huku wananchi waliokuwa wamejaa mkutanoni hapo walisikika wakiitikia 'ndiyooooo....wewe ndiyo rais wetu wa Bundaaaa.'

Alisema tangu alipokuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Vijana-CCM hadi sasa amekuwa mstari wa mbele kupigania maendeleo ya wana Bunda na utatuzi wa kero ya maji, hivyo hatarudi nyuma kamwe wala kukatishwa tamaa kuwatetea wananchi wa jimbo hilo.

Kuhusu kesi ya madai, Mbunge Bulaya ambaye pia ni Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Wazee na Walemavu, aliwaomba wananchi wa Bunda kupitia mkutano huo idhini ya kuwafungulia kesi ama lah, wapinzani wake waliopinga ushindi wake mahakamani, ambapo wananchi hao waliridhia afungue kesi.

Walifungua kesi mahakamani kupinga ushindi wa Bulaya na baadaye kushindwa katika Mahakama ya Rufani ni, wapiga kura wa Jimbo la Bunda Mjini, ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Sariro na Acsetic Malagila.

"Tumemshinda kesi mzee Wassira mara tano....yaani kama ni gori ni tano bila (kicheko na kushangiliwa). Mara ya kwanza tulimshinda mwaka 2015, akaenda mahakamani tumemshinda na wameambiwa na Mahakama kunilipa.

"Na ninyi mliotumiwa ninyi akina Sariro, nyumba zenu tutazipiga mnada. Nitakwenda kukaa na jembe langu Tundu Lissu, tuwafungulie kesi ya madai hawa jamaa. Lazima walipe," alisema Mbunge Bulaya aliyekuwa akishangiliwa na watu mara kwa mara mkutanoni hapo.

        Chadema: 2020 kama Kenya

Katika hatua nyingine, Chadema imemtumia salamu Rais John Magufuli, kikisema kitamshinda kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, kama alivyoshindwa anayedaiwa kuwa raifiki yake Rais Odinga, nchini Kenya.

Akihutubia mkutano huo wa hadhara Mjini Bunda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa (Zanzibar), Salum Mwalim, alisema ushindi alioupata Rais Mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta, dhidi mpinzani wake wa NASA, Odinga utatumika pia kumwangusha Rais Magufuli uchaguzi ujao.

"Tunamwambia Magufuli huyu huyu tutamnyoosha 2020 kama Rais Uhuru Kenyatta, wa Kenya alivyomnyoosha rafiki yake Raila Odinga. Rais Magufuli kutuzuia mikutano ametufanya tutafakari zaidi.

"Ukiona kobe kainama ujuwe anatunga sheria na anatafakari kwa kina. Uhuru Kenyatta, ametoa funzo zuri sana la kidemokrasia....amewaruhusu wapinzani wake kuandamana kupinga ushindi wake. Kenyatta awafundishe wenzake Afrika Mashariki demokrasia, " alisema Mwalim.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, John Heche, pamoja na Mwenyekmiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa wa Mara wa chama hicho, Ester Matiko, walishtumu uminywaji wa haki na demokrasia nchini.

Kwa mujibu wa Heche na Matiko, majimbo na halmashauri zote zinazoongozwa na Chadema zimepata hati safi kutoka serikalini katika usimamizi mzuri wa fedha na maendeleo ya wananchi.

"Pale Tarime kwetu nimeambiwa eti mkurugenzi aanataka kwenda kubomoa madarasa shuleni, sababu yamejengwa na Chadema.

"Namwambia ajaribu aone....kama ni mwanaume atangulie yeye kwenda kubomoa halafu nimshushie wananchi hapo aone kazi yake. Mara ni kwa wanaume bwana," alisema Heche kisha akashangiliwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.