ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, June 8, 2017

WAINGEREZA WASHIRIKI UCHAGUZI MKUU, WABUNGE 650 KUCHAGULIWA.

Mamilioni ya wananchi wa Uingereza hii leo wanaelekea kwenye masanduku ya kupiga kura kushiriki uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, ambapo chama tawala cha Kihafidhina kinatazamiwa kuchuana vikali na chama cha upinzani cha Leba.

Wabunge 650 wanatazamiwa kuchaguliwa katika zoezi hilo, ambapo takriban watu milioni 46.9 wametimiza masharti ya kupiga kura. Chama kitakachozoa kura nyingi kitajipatia fursa ya kuunda serikali ijayo ya Uingereza.

Ushindani mkali uko kati ya chama tawala cha Kihafidhina kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa Theresa May na kile cha upinzani cha Leba kinachoongozwa na Jeremy Corbyn.

Corbyn amekuwa akisisitiza kuwa, ni katika manifesto ya chama chake kulitambua mara moja taifa la Palestina iwapo wataibuka na ushindi katika uchaguzi huu wa mapema, sambamba na kushinikiza kusitishwa mara moja mzingiro wa kibaguzi, ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina na kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.

Thereza May (kulia) na Jeremy Corbyn 
 
Uchaguzi huu unafanyika chini ya anga ya mashambulizi ya kigaidi yaliyoshuhudiwa hivi karibuni katika baadhi ya miji ya nchi hiyo. Shambulizi la hivi karibuni ni lile la Jumamosi iliyopita, ambapo magaidi watatu waliua watu saba katika tukio lililohusisha watu kugongwa na gari na wengine kuchomwa visu jijini London. 
 
Tukio hilo lilitokea majuma kadhaa tu baada ya watu 22 kuuliwa baada ya gaidi kujiripua ndani ya uwanja mmoja wa burudani mjini Manchester.
 
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, uchaguzi huu ulipasa kufanyika mwezi Mei mwaka 2020, lakini mwezi jana Theresa May aliitisha uchaguzi wa kabla ya wakati.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.